PremierBet Ad
Asas Dairies Ad
NBC Ad

Top Stories

Rais Magufuli amtumia Mstaafu Mkapa salamu za rambirambi

on

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Benjamin William Mkapa (Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu) kufuatia kifo cha Makamu Mkuu wa chuo hicho Prof. Egid Beatus Mubofu kilichotokea leo tarehe 18 Desemba, 2018 huko Pretoria, Afrika Kusini.

Prof. Mubofu alipelekwa Jijini Pretoria kwa matibabu zaidi akitokea Taasisi ya Tiba ya Mifupa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MOI) alikokuwa akipatiwa matibabu ya kiharusi.

Rais Magufuli amemuomba Mkapa kufikisha salamu zake za pole kwa familia ya Marehemu Prof. Mubofu, Wahadhiri na wafanyakazi wa UDOM, Wanafunzi wote wa UDOM, Jumuiya na taasisi zote ambazo Prof. Mubofu alifanya kazi na wote walioguswa na msiba huu.

“Nimesikitishwa sana na kifo cha Prof. Mubofu, nitamkumbuka kwa uchapakazi wake, ubunifu, uadilifu na uaminifu mkubwa aliouonesha katika utumishi wake kwa Taifa ikiwemo kazi nzuri aliyoifanya katika Shirika la Viwango la Taifa (TBS) akiwa Mkurugenzi Mkuu, kabla ya kuteuliwa kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha UDOM” Rais Magufuli

Rais Magufuli ameiombea familia ya Marehemu Prof. Mubofu kuwa na moyo wa subira na uvumilivu na amemuombea kwa Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi, Amina.

RAIS MAGUFULI: ‘Nataka mtembee kifua mbele na Kujidai”

 

Soma na hizi

Tupia Comments