Ripota wa TZA nchini Kenya Julius Kipkoech anaripoti kwamba nchi hiyo inarejea kwenye headlines kuhusu maswala ya kubuni sheria za kipekee ambapo sasa bunge la kitaifa linapanga kujadili sheria inayopendekezwa kwamba raia yeyote wa kigeni anayepatikana akishiriki uhusiano wa jinsia moja ahukumiwe kupigwa mawe hadharani hadi kufa na kama ni raia wa Kenya basi ahukumiwe kifungo cha maisha jela.
Mwandishi na mdhamini wa sheria hiyo Edward Onwong’a Nyakeriga anapendekeza kuharamishwa kwa ulawiti na kuhukumiwa jela kwa wanaotenda kosa hilo huku akisisitiza >> ‘upo umuhimu wa kuwalinda watoto na vijana ambao wanalengwa na dhulma ambazo kwa mda mrefu zinaepukwa kutokana na mabadiliko, teknolojia na habari isiyo chujwa na watoto mayatima kukosa mwakilishi pamoja na majaribio ya wanaoshiriki uhusiano wa jinsia moja kuwalea watoto ilihali wanaendeleza uhusiano wao’
Mswada huu wa chama cha Republican Liberty Party unaharamisha uhusiano wowote wa jinsia moja na tayari spika wa Bunge la kitaifa Kenya Justin Muturi ameupokea na kuuwasilisha kwa kamati ya sheria bungeni ambayo inatathmini kisha kutoa ripoti kwa bunge.
Muswada huo pia unapendekeza kupigwa mawe hadharani hadi kufa kwa mtuhumiwa anayepatikana na kosa la kuwalawiti watoto wadogo au anayefanya kitendo hicho na kumuambukiza mtoto virusi vya ukimwi ambapo tayari wabunge 78 wamekubali kuunga mkono muswada huo kuwa sheria na wengine zaidi wanaendelea kushawishiwa.
Haya yanajiri wakati Bunge la kitaifa la Kenya likibuni kikundi mseto cha wabunge kuhusu maisha ya walio katika uhusiano wa jinsia moja na wameahidi kutoa mwelekeo wa jinsi ya kushughulikia jambo hilo huku muswada huu ukitarajiwa kupata upinzani mkali kutoka kwa wanaotetea haki za binadamu.
Mwandishi wa vitabu maarufu nchini Kenya Binyavanga Wainaina amekua miongoni mwa waliojitokeza hadharani na kukiri kushiriki mapenzi ya jinsia moja na wakati huohuo Mashirika ya kutetea haki za wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja hivi karibuni yaliwasilisha pendekezo la kutaka Wabunge kuondoa sheria zote zinazowazuia kuishi maisha yao kama watu wengine.
Katiba ya Kenya mwaka 2010 imeharamisha ndoa ya jinsia moja japo haiharamishi moja kwa moja uhusiano wa mapenzi ya jinsia moja ambapo pia mwezi uliopita utafiti uliofanywa na kampuni ya Ipsos Synovate umeonyesha kwamba 64% ya Wakenya wanaamini kwamba hisia za kushiriki mapenzi na jinsia sawa ni jambo la kujifunza ilihali 14% kati yao wanaamini watu hao huzaliwa walivyo.
Baada ya kuisoma hii stori unaweza kuacha maoni yako kwenye comments hapa chini.