Vita vya Israel na Hamas: Marekani inaripotiwa kuwa iko ukingoni mwa kuidhinisha uuzaji wa silaha kwa Israel, ambayo kama itaidhinishwa, itakuwa mauzo makubwa zaidi ya silaha kuwahi kutokea kwa Israel tangu kuanza kwa vita huko Gaza baada ya Oktoba 7 mwaka jana.’
Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la Washington Post, Wademokrat wawili wakuu katika Bunge la Congress la Marekani wamekubali kuunga mkono uuzaji mkubwa wa silaha kwa Israel unaojumuisha ndege 50 za kivita za F-15 zenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 18. Gazeti la kila siku la Marekani liliripoti huku likiwanukuu maafisa watatu ambao hawakutajwa.
Gazeti hilo liliripoti kuwa Mwakilishi Gregory Meeks na Seneta Ben Cardin wametia saini mkataba huo chini ya shinikizo kubwa kutoka kwa utawala wa Biden.
Kwa miezi kadhaa, wabunge hao wawili walikuwa wameshikilia uuzaji huo huku kukiwa na mzozo wa kibinadamu ambao haujawahi kutokea huko Gaza ambao umesababisha vifo vya zaidi ya 37,000 katika eneo lililozingirwa la Wapalestina.