Robo ya wakazi wa Somalia, au watu milioni 4.3, wako hatarini kukumbwa na njaa ifikapo mwisho wa mwaka, Umoja wa Mataifa umeonya, huku nchi hiyo masikini katika Pembe ya Afrika ikikabiliwa na mafuriko mabaya.
Kwa mujibu wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), mafuriko hayo yameathiri pakubwa jamii ambazo tayari zinatatizika kujikwamua kutokana na ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea katika miongo kadhaa, ambao ulileta mamilioni ya watu kwenye ukingo wa njaa.
Misaada ya kibinadamu hadi sasa imezuia hali ya njaa, lakini kulingana na WFP, Somalia inakabiliwa na viwango vyake vya utapiamlo kwa zaidi ya muongo mmoja.
Kutokana na uhaba wa fedha, wakala wa Umoja wa Mataifa unaweza tu kutoa msaada wa chakula kwa chini ya nusu ya wale wanaohitaji zaidi.
“Lakini huku robo ya wakazi wa Somalia – watu milioni 4.3 – wakitarajiwa kukabiliwa na hali mbaya ya uhaba wa chakula au mbaya zaidi… ifikapo mwisho wa mwaka, msaada kutoka kwa jumuiya ya kibinadamu unasalia kuwa tegemeo,” iliongeza WFP.
Takriban watu 31 wamefariki na wengine 500,000 wamelazimika kuyahama makazi yao nchini Somalia kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zisizokwisha, kulingana na ripoti rasmi Jumapili.
Tangu mwanzoni mwa Novemba, Somalia imekuwa ikikabiliwa na mvua zisizokwisha kutokana na hali ya hewa ya El Niño, ambayo imefurika nyumba na mashamba. El Niño kwa sasa inakuza msimu wa mvua katika Pembe ya Afrika, na madhara makubwa nchini Ethiopia (angalau 20 wamekufa) na Kenya (angalau 15 wamekufa).