Kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha Mkoani Dodoma, nyumba 127 zimebomolewa na mafuriko ambapo watu 493 wamekosa makazi ya kuishi, pia nyumba 240 zimezingirwa na maji katika Kijiji cha Chipogolo Kata ya Chipogolo tarafa ya Rudi Wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma na kusababisha jumla ya wakazi 1390 kukosa makazi ya kuishi.
Naibu Waziri wa Nishati na madini ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kibakwe Wilayani Mpwapwa Mh. George Boniface SimbaChawene amesema katika kikao cha tathmini kilichofanyika mara baada ya kukagua eneo lililoathilika na mafuriko, wamekubaliana hatua mbalimbali zichukuliwe ikiwemo kujenga upya madaraja yaliyopo pamoja na kuongeza kimo na urefu wa madaraja hayo kwa kuwa madaraja yaliyopo ni mafupi na yanazidiwa na maji.
Pia Mbunge huyo ameiomba kamati ya maafa kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba wakazi wa kijiji hicho wanapata huduma mbalimbali zikiwemo za Afya kwa kuwapa madawa, elimu pamoja na kuwaongezea wataalamu wa afya, kuwapatia Mahema, mablaketi na magodoro na chakula.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mh. Christopher Ryoba Kangoye amewaomba wakazi wa kijiji hicho kuendelea kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu wakati serikali kupitia kamati ya maafa Mkoa wa Dodoma ikiendelea kushughulikias matatizo yao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi David A. Misime amewataadharisha wakazi wa kijiji hicho kuwa watulivu kwani matatizo kama haya hayatatuliwi kwa vurugu badala yake watumie vikao vinavyostahili kutatua matatizo yao “matatizo kama haya hayatatuliwi kwa kufanya fujo na kufunga barabara”
Wakati huohuo Kituo cha Polisi Kata ya Chipogolo na nyumba tano za Askari wa kituo hicho zimeanguka kutokana na mafuriko hayo, Kamanda Misime ametoa pole kwa Askari wa kituo hicho na kuwasisitiza waendelee kufanya kazi kwa maadili ya Jeshi bila kujali wakati tatizo lao linashughulikiwa na mamlaka husika kwani vituo vya Polisi kama hivyo vipo chini ya Mkurugenzi na wananchi kwakuwa vilijengwa kwa nguvu zao.
Stori imeandaliwa na Sylvester Onesmo wa Jeshi la Polisi Dodoma .