Kufuatia kuwepo kwa hoja mbalimbali za wajumbe wa Bunge maalum la katiba kuhusu kukinzana kwa Hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa wakati wa uzinduzi wa bunge hilo na rasimu ya katiba iliyowasilishwa na mwenyekiti wa tume ya mabadiliko ya katiba jaji Joseph Warioba, mwenyekiti wa bunge maalum Samwel Sitta ameridhia kujadiliwa kwa hotuba hizo.
Amesema baada ya kutolewa kwa hotuba hizo amekuwa akipokea maombi ya Wajumbe mbalimbali wakishauri kutaka zijadiliwe na kupendekeza mjadala huo ufanyike siku ya Jumatano wiki hii.
Kauli ya Mwenyekiti huyo imetokana na muongozo ulioombwa na mmoja wa wajumbe wa Bunge hilo Julius Mtatiro aliyetaka mwenyekiti wa tume ya mabadiliko ya katiba Jaji Joseph Warioba aitwe bungeni kujibu baadhi ya hoja zilizotolewa na Rais kikwete ambazo zinapingana na rasimu iliyowasilishwa.
Namkariri Mtatiro akiuliza ‘kwa sababu Rais alikaribishwa tu kwa heshima kwenye bunge hili kuja kufungua na sasa akaanza kujibu ile hotuba, hatuoni kama kuna haja ya kujenga utaratibu wa kumleta tena mtoa hoja ili na yeye aje kujenga hoja juu ya maswali aliyoeleza Rais?’
Kwenye sentensi nyingine mwenyekiti wa Bunge hili maalum la katiba Samwel Sitta ameunda kamati 12 zitakazokuwa zikijadiliana kuhusu ibara za katiba zitakazopangwa kwa ajili ya kuwasilishwa bungeni kwa mijadala ya jumla.