Mamlaka nchini Tajikistan, inasema karibia watu kumi na wawili wamefariki kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha kwenye taifa hilo.
Vifo hivyo vimeripotiwa katika miji mitatu jirani na jiji kuu la Dushanbe, baada ya mvua kubwa kunyesha siku ya Jumapili na kusababisha mafuriko na maporomoko ya udongo.
Kwa mujibu wa msemaji wa idara ya masuala ya dharura nchini humo, idadi hiyo imeongezeka kutoka kwa ile ya watu 13 waliokuwa wamefariki siku ya Jumatatu.
Tajikistan, ni taifa maskini katikati mwa Asia na limekuwa likikabiliwa na majanga tofauti ya kiasili.
Mwezi Februari maporomoko ya udongo yaliripotiwa katika eneo la Badakhshan, mpaka na mataifa ya Afghanistan, China na Kyrgyzstan.