Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Kanda ya Mashariki Caroline Malundo, amewataka wananchi kuachana na shughuli za uharibifu wa mazingira na badala yake wajikite katika kutunza misitu ili kuongeza watali na kukuza uchumi kupitia utalii.
Kamanda Caroline amebainisha hayo wakati wa ofa ya msimu wa nanenane kutembelea maporomoko ya maji ya hululu katika Milima ya uluguru hifadhi inayosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), ambapo amesema mamlaka za uhifadhi zimekuwa zikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha jamii inashiriki katika uhifadhi wa mazingira, mpango ni wananchi kutumia maji yanayotiririka kukua kiuchumi kupitia kilimo.
Watalii zaidi ya 30 waliofika kwenye maporomoko hayo ya maji , wamevutiwa na namna wakazi wa vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo wanavyothamini na kutunza mazingira.
Pamoja na hifadhi hiyo kusimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), wakazi hao wanasema zipo sheria ambazo wamejiwekea katika kuhakikisha mazingira hayo yanaendelea kuwavutia watalii kufika eneo, changamoto ni mahitaji ya nishati ya kupikia kuwafanya baadhi yao kukiuka taratibu zilizowekwa.