Makundi ya kiraia katika eneo hilo yamesema, raia 16 wameuawa katika wimbi hilo la mashambulizi ya makombora, maroketi na ufyatuaji risasi dhidi ya makazi ya raia katika eneo la Ombada, kaskazini magharibi mwa Khartoum jana Jumanne.
Mohamed Mansour, mkazi wa eneo hilo amenukuliwa na shirika la habari la AFP akisema kuwa, binafsi ameshuhudia maiti 8 zikiondolewa kwenye vifusi vya jengo moja lililoripuliwa. Mkazi mwingine Hagar Yusuf naye amesema watu wanne wakiwemo watoto wawili wameuawa katika hujuma iliyolenga jengo lililo jirani yake.
Makundi yanayopigania demokrasia yanayojiita ‘Kamati za Mapambano’ yamesema idadi hasa ya watu waliouawa kwenye mashambulizi hayo ya jana haijajulikana kufikia sasa, kwa kuwa miili yote haijaondolewa kwenye vifusi vya majengo yaliyoshambuliwa.
Mashambulizi hayo yamejiri wakati huu ambapo mapigano yaliyozuka katikati ya mwezi wa Aprili kati ya pande zinazoongozwa na majenerali hasimu nchini Sudan wanaowania madaraka, wa Jeshi na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka RSF yakipamba moto.
Hii ni katika hali ambayo, siku chache baada ya raia wasiopungua 20 waliuawa katika shambulio la roketi lililolenga maeneo ya makazi ya raia kwenye moja ya miji mikubwa ya jimbo la Darfur na jengine la makombora lililotokea karibu na hospitali kadhaa katika jimbo la Kordofan Kaskazini.
Kulingana na makadirio yasiyo rasmi, vita na mapigano yaliyozuka Aprili 15 katika mji mkuu Khartoum na kuenea hadi Darfur baadaye mwezi huo, yamesha sababisha hadi sasa vifo vya watu wasiopungua 3,900 kote nchini Sudan.