Jeshi la UPDF la Uganda na jeshi la FARDC la DRC katika operesheni yao ya pamoja yamewaokoa watu 19 waliotekwa nyara na waasi wa kikosi cha ADF katika mkoa wa Ituri nchini DRC unaopakana na Uganda.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Meja Bilal Katamba, afisa wa habari za umma wa Kitengo cha Mlimani cha UPDF, waliookolewa ni pamoja na watoto wanane, wanawake tisa na wanaume wawili, ambao waliripotiwa jumamosi iliyopita katika kambi ya pamoja ya Bwakadde mkoani Ituri baada ya majeshi hayo kushambulia kituo cha ADF katika vilima vya Tingwe, kaskazini mashariki mwa wilaya ya Erengeti ya DRC.
Taarifa hiyo pia imesema, watu hao 19 wamesafirishwa kwa ndege na UPDF na kupatiwa matibabu na timu ya madaktari wa UPDF. Majeshi hayo yanaendelea kuwasaka waasi.
Wakati huo huo, viongozi wa kimila na mitaa katika jimbo la Ituri wameahidi kuunga mkono vikosi vya pamoja ili kuhakikisha kuwa amani kamili inapatikana katika jimbo hilo.
Hii ilikuwa wakati Kamanda wa Vikosi vya Nchi Kavu, Luteni Jenerali Kayanja Muhanga akitoa wito kwa machifu wa Ituri alipotembelea kambi mbalimbali za vikosi vya pamoja katika jimbo hilo.