Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imetoa elimu ya fedha na umuhimu wa uwekaji akiba kwa wanafunzi na walimu wa Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Pugu iliyopo Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam.
Hatua hiyo inalenga kutoa fursa kwa wanafunzi hao kujifunza masuala ya kifedha ili kuwajengea utamaduni wa kujiwekea akiba, kubuni mawazo ya biashara sambamba na kutambua namna ya kutumia taasisi za kifedha ikiwemo benki hiyo ili kujinufaisha kiuchumi.
Semina fupi kuhusu mafunzo hayo ilifanyika mwishoni mwa wiki shuleni hapo ikiongozwa na Mkuu wa Kitengo cha Uhakiki vigezo (Compliance) NBC Bi Sarah Laiser, aliyeambatana na viongozi wengine waandamizi wa benki hiyo akiwemo Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja wa Benki ya NBC, Salama Mussa, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ukaguzi wa Mahesabu wa benki ya NBC, Fulgence Shiraji pamoja na maofisa wengine waandamizi.
Wenyeji waliongozwa na Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Boniface Orenda, baadhi ya walimu pamoja na wanafunzi.
Akizungumzia hatua hiyo Laiser alisema ni muhimu kwa kuwa inalenga kuwajengea ufahamu na ujuzi wa kifedha vijana hao wakiwemo wale wanaotarajia kuhitimu elimu ya sekondari na kujiunga elimu ya juu na wale watakaojiri.
“Elimu ya fedha kwa wanafunzi ni muhimu kwa sababu inawawezesha kuelewa mapema jinsi ya kutunza na kuendesha fedha zao, kubuni na kufuata bajeti, na kufanya maamuzi sahihi ya kifedha.’’
“Zaidi, uwepo wetu hapa leo unalenga kuwasaidia wanafunzi hawa kutambua umuhimu wa akiba, uwekezaji, na matumizi sahihi ya mikopo.
“Tunaamini hawa ndio wajasiriamali, wawekezaji na maofisa wa kesho hivyo ni vema kuanza kuwaandaa mapema ili pia waweze kujua namna ya kutumia taasisi za fedha katika kujikwamua.’’
Wakiwa shuleni hapo maofisa wa benki hiyo walipata wasaa wa kutoa mafunzo na kuwasilisha mada mbalimbali kuhusu masuala ya fedha, ujasiriamali pamoja na kutoa fursa kwa wanafunzi hao wakiwemo wale wenye mahitaji maalum kujibu na kujadili hoja mbalimbali kuhusu mada hizo.
“Pia tumepata fursa ya kutambulisha huduma zetu mahususi kwa wanafunzi na walimu zikiwemo akaunti za Mwanafunzi na akaunti ya Mwalimu zilizobuniwa kulingana na mahitaji ya makundi hayo.
“Pia tumetoa zawadi mbalimbali ikiwemo jezi za vilabu vinavyoshiriki ligi kuu ya NBC Premier League, mipira na zawadi binafsi zilikabidhiwa kwa uongozi wa shule pamoja na wanafunzi mbalimbali. ‘’ aliongeza.
Zaidi, maafisa hao, walishiriki zoezi la upandaji miti ya matunda na vivuli kwenye viunga vya shule hiyo ili kuacha kumbukumbu pamoja na kuunga mkono jitihada za shule hiyo pamoja na serikali katika utunzaji wa mazingira.
Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Orenda, pamoja na kuishukuru Benki ya NBC kwa hatua hiyo, alisema elimu hiyo itawasaidia wanafunzi hususani wale wanaotarajia kuhitimu kuwa na elimu ya kujiwekea akiba, kujijenga kijasiriamali hata pale watakaposhindwa kuendelea na elimu ya juu zaidi.
“Kimsingi ujio wa NBC shuleni hapa umekuwa na tija kubwa si tu kwa wanafunzi bali pia walimu kwa kuwa huduma zao zinatulenga pia walimu. Elimu hii imewanufaisha jumla ya wanafunzi 930 wanaosoma hapa ambapo 139 kati yao ni wenye mahitaji maalum.
Tunashukuru mafunzo yamekuwa shirikishi kwa wanafunzi wa aina zote wakiwemo wenye mahitaji maalum na wote wameweza kujibu maswali kwa ufasaha na wamepata zawadi,’’ alisema.
Kwa mujibu wa Mwalimu Orenda, umuhimu wa elimu ya fedha kwa wanafunzi hao unaokana zaidi pindi wanapohitimu elimu yao ambapo baadhi yao hujiingiza kwenye shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo biashara na hata wanaondelea na elimu ya juu, bado elimu ya fedha imekuwa ikiwasaidia katika kufanya maamuzi yanayohusu fedha wanazozipata ikiwemo mikopo ya elimu ya juu na pesa wanazotumiwa na wazazi pamoja na walezi wao wakiwa vyuoni.