Rais wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati aliye uhamishoni Francois Bozize, ambaye sasa anaongoza muungano wa waasi, amehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kula njama, uasi na mauaji katika taifa hilo ambalo halijatulia kwa muda mrefu.
Bozize, ambaye alichukua mamlaka nchini CAR mwaka 2003 lakini akapinduliwa muongo mmoja baadaye, alihukumiwa bila kuwepo mahakamani siku ya Alhamisi, kulingana na hukumu iliyotumwa kwa AFP na wizara hiyo.
Watoto wawili wakubwa wa Bozize pamoja na watuhumiwa wengine 20 wakiwemo viongozi wa waasi, pia walihukumiwa adhabu kama hiyo bila ya wao kuwepo mahakamani.
Pia walipatikana na hatia ya kuathiri usalama wa ndani na “mauaji”, kulingana na hukumu ya mahakama ya rufaa katika mji mkuu wa Bangui.
Hukumu haikutoa maelezo juu ya muda uliohusika au uhalifu.
Mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yamekuwa yakishuhudiwa nchini Jamhuri ya Afrika ya kati mojawapo ya mataifa maskini zaidi duniani tangu mwaka wa 2013.
Bozize, 76, ambaye alikuwa uhamishoni nchini Chad hadi Machi alipohamia Guinea Bissau, anaongoza muungano wa makundi ya waasi yanayoitwa Coalition of Patriots for Change (CPC), yaliyoundwa Desemba 2020 kwa nia ya kumpindua mrithi wa Bozize, Faustin Archange. Touadera.