Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umesema umefanikiwa kupunguza na kuondoa ada za huduma mbalimbali ili kupunguza urasimu katika shughuli zao, ambapo wamefanikiwa kuondoa na kupunguza jumla ya ada 13 ikiwa ni pamoja na kuondoa ada ya usajili wa eneo la kazi iliyokuwa ikitozwa kati ya shilingi 50,000 hadi 1, 800,000, kufuta faini zinazohusiana na kukosekana kwa vifaa vya kuzimia moto ya shilingi 500,000 hiyo yote ikiwa ni kuhakikisha wanaboresha mazingira ya Watu kufanya kazi na kujali usalama wa Wafanyakazi wakiwa maeneo ya kazi,”-
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda amesema hayo akiwa Jijini Dar es salaam “OSHA kama Taasisi wezeshi, tulifanya mapitio ya mlolongo wa shughuli zetu (Business Process Review) na kubaini maeneo yaliyohitaji maboresho katika utoaji wa huduma, miongoni mwa maeneo yaliyoonekana kuwa na uhitaji wa maboresho ilikuwa ni kupunguza au kuondoa baadhi ya ada za huduma ambazo zisingeathiri usimamizi na utoaji wa huduma za usalama na afya mahali pa kazi nchini”
“Kingine kilichofanyika ni kuondoa ada ya fomu ya usajili sehemu za kazi iliyokuwa ikitozwa Sh. 2,000, kufuta faini zinazohusiana na ukosefu wa vifaa vya kuzimia moto ya Sh. 500,000, kuondoa ada ya leseni ya Ithibati iliyokuwa inatozwa Sh 200,000 kwa mwaka”
“Kuondoa ada ya ushauri wa kitaalamu wa Usalama na Afya ya Sh 450,000, kufuta ada ya mafunzo ya elimu kwa umma iliyokuwa inatozwa kiasi cha Sh. 250,000 kwa kila Mshiriki”
“Kupunguza ada ya uchunguzi wa ajali iliyokuwa ikitozwa Sh. 500,000 mpaka Sh. 120,000, kuondoa ada ya Kipimo cha Mzio (Allergy test) iliyokuwa ikitozwa Sh. 25,000 kwa Mfanyakazi, kuondoa ada ya Kipimo cha Kilele cha Upumuaji (Peek Expiratory Flow test) iliyokuwa ikitozwa Sh. 10,000 kwa Mfanyakazi”
“Kupunguza ada ya huduma za ukaguzi wa mifumo ya umeme katika vituo vya mafuta vilivyopo vijijini kutoka Sh. 650,000 hadi Sh. 150,000, punguzo hili lililenga kuhamasisha uwekezaji katika maeneo hayo”
“Hivyo, kupunguza athari zinazoweza kutokea kutokana na utunzaji wa mafuta kwenye chupa za maji na madumu, suala ambalo linahatarisha maisha ya wananchi katika maeneo hayo, kuondoa ada ya ukaguzi wa usimikaji wa pampu za gesi kwa kila kituo ambayo ilikuwa inatozwa Sh. 20,000 kwa kila pampu.
Hivyo, ni dhahiri kuwa ada zilizofutwa ama kupunguzwa na OSHA zimeleta unafuu ambao umechochea ukuaji wa biashara na uwekezaji nchini ikiwemo kuongeza ajira kwa Watanzania. Ada zilizofutwa ama kupunguzwa zinakadiriwa kuwa zaidi ya Shiling Bilioni 35 ambapo imempendeza Mhe. Rais fedha hizo zitumike katika kuimarisha mifumo ya kulinda wafanyakazi ili waweze kuzalisha kwa tija.