Polisi walipekua ofisi ya Brussels ya mbunge wa Bunge la Ulaya Maximilian Krah kuhusu madai ya ujasusi ya China, mamlaka ya Ujerumani ilisema Jumanne.
Waendesha mashtaka wa serikali walisema ofisi ya Krah katika Bunge la Ulaya ilipekuliwa asubuhi kama sehemu ya uchunguzi kuhusu msaidizi wake wa bunge Jian G., ambaye anatuhumiwa kuwa “mfanyakazi wa huduma ya siri ya China.”
Jian G. alikamatwa mwezi uliopita kwa tuhuma za kufanya shughuli za kijasusi katika Bunge la Ulaya, na kupitisha taarifa nyeti kwa China, madai yaliyokanushwa na Beijing.
Waendesha mashtaka wa Ujerumani walisema msako huo ulifanyika baada ya Bunge la Ulaya kuwaruhusu kuingia ndani ya jengo hilo. Polisi wa Brussels waliongoza msako huo, huku mamlaka za Ujerumani zikifuatilia.
Maximilian Krah, mtu maarufu wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha AfD, anagombea kama mgombea mkuu katika uchaguzi wa mwezi ujao wa Bunge la Ulaya. Krah alisema mwezi uliopita kuwa atakatisha mkataba wa msaidizi wake, lakini akafutilia mbali kujiuzulu kutokana na tukio hilo.