Kampeni za uchaguzi mkuu zimemalizika usiku wa manane siku ya Jumapili. Wapiga kura milioni 5.3 wameitwa kupiga kura siku ya Jumatano Oktoba 9 kumchagua rais mpya na wajumbe wa mabunge ya majimbo.
Rais anayemaliza muda wake, Filipe Nyusi, kutoka chama cha FRELIMO, hatowania katika uchaguzi huo baada ya kuhudumu mihula miwili.
Wagombea wanne wanagombea kwenye nafasi hii.
Ni uchaguzi ambao mgombea wa chama tawama Daniel Chapo, mtangazaji wa zamani na mhadhiri wa sheria, anatarajiwa kumrithi rais Filipe Jacinto Nyusi.
Hata hivyo masuala kadhaa yanatazamwa na wagombea ikiwemo vita dhidi ya makundi ya kijihadi kaskazini mwa nchi hiyo, ambapo maelfu ya raia wameuawa na wengine kukimbia makazi yao kwenye jimbo la cabo Delgado tangu mwaka 2017.
Aidha agenda ya kufufua uchumi kupitia miradi ya gezi ni suala jingine linalozungumzwa na raia, ambapo tangu kuzuka kwa uasi kaskazini mwa nchi hiyo, miradi yenye thamani ya karibu dola bilioni 50 ilisimama, kampuni ya kifaransa ya mafuta TotalErnergies ikilazimika kufunga kabisa opereshen zake nchini humo.