Ukraine imesema mapema Jumatatu kwamba vikosi vyake vimekishambulia kituo cha mafuta katika eneo la Crimea linalodhibitiwa na Urusi tangu mwaka 2014.
Mamlaka zilizowekwa na Urusi huko Crimea zilisema shambulizi lilisababisha kuzuka kwa moto katika ghala la mafuta katika mji wa bandari wa Bahari Nyeusi wenye watu 70,000 lakini hakukuwa na majeruhi walioripotiwa.
Wizara ya ulinzi ya Urusi wakati huohuo ilisema kuwa droni 12 kati ya 21 za Ukraine zilizorushwa usiku kucha zilidunguliwa.
Ukraine imesema mashambulizi hayo ni kisasi cha haki kwa mashambulizi ya Urusi kwenye miundombinu yake ya nishati ambayo yamewaingiza mamilioni gizani.
Kyiv imeongeza mashambulizi yanayolenga sekta ya nishati ya Urusi katika miezi ya hivi karibuni ikiamini kwamba maeneo hayo ndiyo yanaipatia Urusi jeuri ya mapato na kuendeleza uvamizi wake nchini Ukraine ambao unapindukia mwaka wa tatu.