Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango ametoa siku saba kwa Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuhakikisha wanatatua changamoto inayokwamisha ujenzi wa Barabara ya Pangani – Makurunge Bagamoyo ambayo imekwama kutokana na eneo la jiwe la kuchimba kokoto leseni yake ya uchimbaji kupewa Mtu mwingine tofauti na Mkandarasi husika.
Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 19 Novemba 2022 wakati aliposimama kuzungumza na Wananchi wa Mkata Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga akiwa njiani kuelekea makao makuu ya mkoa huo kwa ajili ya ziara.
Ameagiza Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kuhakikisha wanafanyia kazi mapema zaidi maeneo yanayotumika kwaajili ya ujenzi wanayoyapata baada ya tafiti wanazofanya ili kuepusha migogoro inayokwamisha maendeleo ya miradi.
Pia ameagiza kutatuliwa mara moja changamoto iliokwamisha ujenzi wa Barabara ya Handeni – Kibirashi – Kiteto hadi Dodoma ambayo ujenzi wake ulipaswa kuanza tangu mwezi Mei mwaka huu.