Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence amewaongoza Maafisa na askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania pamoja na Watumishi wa Umma katika mapokezi ya ndege ya usafirishaji ambayo imetolewa kwa JWTZ na Jeshi la Umoja wa Falme za Kiarabu.
Akiongea na Maafisa na askari waliohudhuria mapokezi ya ndege hiyo katika viwanja vya Kikosi cha Usafirishaji wa anga Ukonga Jijini Dar es Salaam, Waziri Tax amesema kuwa ndege hii ni msaada ulioamabatana na mafunzo kwa marubani wa JWTZ na akawapongeza wote waliobahatika kupata mafunzo hayo kwa kufanya mafunzo hayo kwa weledi mkubwa.
“Msaada huu unaimarisha uhusiano wa kirafiki baina ya mataifa yetu mawili huku pia ukiongeza uwezo wa Jeshi letu la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania katika kukabiliana na changamoto za kiulinzi na kiusalama zinazohitaji katika mahusiano ya kimataifa” alisema Waziri wa Ulinzi na JKT, Dkt Stergomena Tax.
Aidha, Waziri Tax akasisitiza kuwa Ndege hii itasaidia kutekeleza majukumu ya kijeshi ndani na nje ya nchi, hasa katika shughuli za usafirishaji wa kijeshi na operesheni mbalimbali zikiwemo operesheni za kiraia.
Waziri wa Ulinzi na JKT akaongeza na kusisitiza kuwa upokeaji wa ndege hiyo ni mwendelezo wa uthibitisho wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, katika kuimarisha Ulinzi na Usalama wa Taifa na kuliboresha Jeshi letu la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa vifaa vya kisasa ili kukabiliana na changamoto zinazobadilika kila siku.
Hafla hiyo ya mapokezi ya ndege hiyo pia ilihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na JKT Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, Mnadhimu Mkuu wa Jeshi Luteni Jenerali Salum Haji Othman, Balozi wa Tanzania Falme za Kiarabu Luteni Jenerali (Mstaafu) Yacoub Mohamed,na Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Anga Meja Jenerali Shaban Baraghashi Mani,pamoja na Maafisa Wakuu, Maafisa wadogo, askari na watumishi wa Umma.