Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu inatarajia kutoa uamuzi wa kufuta ama kutofuta dhamana ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, November 23,2018.
Hatua hiyo inatokana na washtakiwa hao kujisalimisha mahakamani hapo na kujieleza kwanini wasifutiwe dhamana, baada ya mahakama hiyo kuamuru wakamatwe na kufikishwa mahakamani hapo ili wajieleze.
Uamuzi huo unatarajia kutolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri baada ya kusikiliza hoja za washtakiwa hao pamoja na maelezo ya upande wa mawakili wa utetezi na wa mashtaka.
Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Mashauri amepanga November 23, 2018 kutoa uamuzi kama awafutie dhamana washtakiwa hao ama lah. Pia mahakama hiyo imetoa nafasi ya mwisho kwa kumpa siku 5 Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa kutafutwa wakili wa kumtetea.
Mbali na Mbowe, Msigwa na Matiko, washtakiwa wengine ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya, na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Vincent Mashinji.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki , kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018, Dar es Salaam.