Upelelezi wa kesi ya utakatishaji fedha wa Dola za Kimarekani 9,018 inayomkabili Mfanyabiashara, Akram Azizi Abdul Rasool ambaye anadaiwa kuwa ni mdogo wa Rostam Aziz bado haujakamilika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Hayo yameelezwa na Wakili wa Serikali, Elia Athanas mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Augustine Rwezire wakati shauri hilo lilipoitishwa kwa ajili ya kutajwa.
Wakili Athanas amedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo anaomba kesi iahirishwe.Baada ya kueleza hayo kesi imeahirishwa hadi November 26, 2018 mshtakiwa anaendelea kusota rumande.
Mfanyabiashara huyo anakabiliwa na mashtaka 75 ya kesi ya uhujumu namba 82/2018 ambapo katika makosa yake, mawili ni kukutwa na Nyara za serikali, kukutwa silaha makosa 70, kukutwa na risasi makosa mawili ambazo ni zaidi ya (6496) na utakatishaji fedha 1.
Miongoni mwa mashtaka aliyosomewa ni kukutwa na nyara za serikali, ambapo anadaiwa amelitenda October 30, 2018 maeneo ya Oysterbay Dar es Salaam ambapo alikutwa na Meno 6 ya Tembo yakiwa na thamani ya Shilingi MIL 103.
Pia anakabiliwa na kosa la kukutwa na nyama ya Nyati, Kilogramu 65 yenye thamani ya Shilingi Mil 4.35 bila kuwa na kibali, ambalo amelitenda October 30,2018 sawa Oysterbay Kinondoni Dar es Salaam.