Mashahidi 15 kutokea Upande wa Mashtaka wanatarajiwa kutoa ushahidi wao katika kesi ya uchochezi inayomkabili mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe.
Hayo yameelezwa na Wakili Serikali, Wankyo Simon mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya kumaliza kumsomea Zitto maelezo ya awali (Ph).
Wakili Katuga amedai kuwa watakuwa na mashahidi 15 na vielelezo ambavyo vinaweza kuwa vya kimaandishi na kielektroniki.
Amedai kuwa jinsi kesi itakavyoendelea kusikilizwa wanaweza kuongeza mashahidi na vielelezo au kupunguza mashidi, kwa sababu hata baada ya Zitto kusomewa maelezo hayo na kuyajibu wanaweza kuwapunguza kutoka 18 hadi 15.
Awali Zitto akisomewa (Ph) na Wakili Simon amedai October 28, 2018 mshtakiwa akiwa katika mkutano na waandishi wa habari, uliyofanyika katika Makao Mkuu ya ofisi ya Chama cha ACT-Wazalendo alitoa maneno ya uchochezi yenye kuleta hisia ya hofu na chuki.
Alidai kuwa Zitto alianza kwa kudai kuwa, ” Watu ambao walikuwa ni majeruni katika tukio la mapambano baina ya wananchi na polisi wakiwa wamekwenda hospital kupata matibabu katika kituo cha afya Nguruka, Polisi wakapata taarifa kuwa kuna watu wanne wamekwenda hospital kituo cha afya Nguruka kupata matibabu wakawafuata kule wakawaua”
Kutokana na maneno hayo, Zitto alikamatwa October 30, mwaka huu akiwa nyumbani kwake Masaki na kuwekwa mahabausu ya polisi na pia nakala ya taarifa ya vyombo vya habari polisi wali ikuchukua baada ya kuwa Zitto amekamatwa.
Baada ya Saimon kumaliza kumsomea maelezo hayo, Zitto alikubali majina yake, alikubali kuwa yeye ni Mbunge na pia alikubali kuwa alikamatwa nyumbani kwake Masaki. Hata hivyo alikataa kuwa yeye si Mwenyekiti wa ACT Wazalendo na nakala ya taarifa hiyo haikukutwa nyumbani kwake wakati anakamatwa.
Pia, alikaa maelezo mengine yote aliyosomewa.Kesi imeahirishwa hadi January 14, 2019 kwa kutajwa na itaendelea kusikilizwa January 29,2019.