AyoTV

Madini ya BILIONI 2 yataifishwa na mahakama, waliokutwa nayo wahukumiwa

on

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeamuru madini yenye thamani ya Sh. Bilioni 2.5 yataifishwe na kuwa mali ya serikali kwani ukwepaji wa kodi ya mrabaha unasababisha taifa likose mapato.

Pia mahakama imeamuru wafanyabiashara watatu wa madini wakiwemo Raia wawili wa China na mmoja wa India kulipa faini ya Shilingi Milioni moja kila mmoja au kutumikia kifungo cha miezi miwili jela kila mmoja.

Wafanyabiashara hao ni Chang Xu, Kai Jiang, Ashok Lavingia na Kampuni ya Sino Africa Collection Ltd ambao walikuwa wakikabiliwa na mashitaka matano ikiwemo ya kuwasilisha taarifa za uongo kwa Kamishna wa madini kwa lengo la kukwepa malipo sahihi ya mirahaba.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi ambapo amesema washitakiwa wanatiwa hatiani kwa kukiri kosa na kwamba katika kila kosa kila mshitakiwa atatakiwa kulipa Sh. 200,000 na kifungo cha miezi miwili ambapo jumla ni Sh. Milioni nne na kifungo cha miezi miwili.

“Mahakama ipo kwa ajili ya kulinda rasilimali za nchi na kwa vitendo mlivyovifanya vinasababisha serikali kukosa mapato. Lakini kwa kuzingatia washitakiwa ni wakosaji wa kwanza,” alisema Hakimu Shaidi.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali, Jacqueline Nyantori aliiomba mahakama kutaifisha madini hayo chini ya Sheria ya Madini inayosomwa sambamba na sheria ya Uwazi na Uwajibikaji ya mwaka 2015.

Wakili wa utetezi, John Gamanya na Flora Jacob wamedai washitakiwa hao ni wakosaji wa kwanza na ni wafanyabiashara wenye vibali hivyo aliomba mahakama izingatie kuwapunguzia adhabu.

Miongoni mwa mashitaka yao, wanadaiwa kati ya June Mosi, 2018 na October 3, mwaka huu maeneo ya jiji la Dar es Salaam, waliratibu na kufadhili biashara iliyofanywa genge haramu kwa lengo la kuchuma faida.

ALIETEULIWA NA RAIS MAGUFULI AZUNGUMZA BAADA YA KUAPISHWA NA BOSS WAKE

EXCLUSIVE: MISS TANZANIA AFUNGUKA BAADA YA KUTOKA MISS WORLD, AZUNGUMZIA ALICHOKIPATA

Soma na hizi

Tupia Comments