NIPASHE
Utafiti uliofanywa na Benki Kuu ya Dunia kwa robo ya kwanza ya mwaka kuhusu hali ya kiuchumi barani Afrika, umeonyesha kuwa Tanzania ni kati ya nchi barani humo ambazo bado zipo imara kiuchumi ndani ya kipindi hicho.
Hata hivyo, baadhi ya nchi zikiwamo zinazozalisha na kusafirisha kwa wingi nje bidhaa ya mafuta, zinatarajia kuonja makali ya mdodoro wa uchumi ndani ya mataifa hayo tangu kipindi hiki hadi mwaka ujao.
Matokeo ya utafiti huo kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2015, yaliyotolewa jana na taasisi hiyo ya fedha duniani kwa kurushwa moja kwa moja kwa nchi zote zilizopo kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwamo , kutoka Washington DC, Marekani.
Akitoa taarifa hiyo, Mchumi kiongozi wa Benki ya Dunia (WB), kwa upande wa Bara la Afrika, Punan Chuhan, alitaja nchi ambazo zinajimudu kiuchumi mpaka sasa kuwa ni Ivory Coast, Tanzania na Msumbiji.
Alitaja baadhi ya sababu kwa nchi hizo hasa Tanzania kubaki katika hali nzuri wakati nyingine zikiteseka, kuwa ni miundombinu imara na utengemavu katika shuguli za uchimbaji wa madini.
Hata hivyo, huo wa kwanza kutolewa na benki hiyo ya dunia barani humo kwa mwaka huu kulingana na utaratibu wake, inaonyesha kuwa hali ya uchumi kwa ujumla barani humo imeshuka kutoka asilimia 4.5 mwaka uliopita hadi asilimia 4 mwaka huu.
NIPASHE
Zaidi ya akinamama wajawazito 70 katika kituo cha Afya cha Chikande, Manispaa ya Dodoma wameandamana hadi Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma kulalamikia mambo mbalimbali.
Malalamiko yao ni pamoja na kujifungulia njiani kutokana na kutembea umbali mrefu kwenda hospitali hiyo na baadhi yao kukataliwa kufunguliwa geti na walinzi wa hospitali wanapojisikia uchungu.
Martha Masine, alisema wameamua kuandamana ili kuwasilisha kilio chao kwa uongozi wa hospitali hiyo ili matatizo yao yatafutiwe ufumbuzi.
“Walinzi wa hospitali ya mkoa wamekuwa wakikataa kuwafungulia geti akina mama wanaofika hospitalini hapo usiku wakitokea Chikande na kusababisha baadhi ya wenzetu kujifungulia njiani na kuhatarisha maisha ya mama na mtoto anayezaliwa,” Masine.
Alisema wamekuwa wakipata shida sana kufika hospitali hapo usiku, ingawa kituo hicho kipo nyuma ya hospitali.
Aidha, alisema wamekuwa wakisindikizana mmoja wao anaposhikwa na uchungu, lakini wanapofika hospitalini walinzi wanagoma kufungua mageti na kuwalazimu kurudi kituoni.
Alibainisha kwa nyakati mbili tofauti akiwa bado katika kituo hicho ameshuhudia akina mama wawili kujifungulia njiani kwa kutembea umbali mrefu kufuata huduma na mwingine kukataliwa na walinzi.
“Bado nipo katika kituo hiki nasubiria kujifungua, muda bado haujafika, lakini jamani sisi tunapata shida walinzi wa General wanapotukatalia kufungua mageti, huwa inatulazimu kuanza safari ya kurudi kituoni na kuna siku tukiwa njiani mwenzetu akajifungua tukamsaidia sisi tuliopo,” Masine.
Rose Atanas ambaye yupo katika kituo hicho akisubiria kujifungua, alisema changamoto nyingine ni kituo hicho kuzidiwa uwezo kutokana na kupokea akina mama wengi kutoka vijiji mbalimbali vya Mkoa wa Dodoma.
“Kituoni kuna kinamama wengi kuzidi uwezo wake, kituo kina vitanda 15 na hadi sasa kuna akinamama zaidi ya mia moja hali inayotulazimu kulala wawili wawili au watatu na wengine kulala chini na pia kuna wadudu watambaao kama vile kunguni na papasi,”Atanas.
Alisema mbali na mrundikano huo pia unahatarisha afya zao na unatishia kuambulizwa na magonjwa ya kuambukiza.
“Pia tuna vyakula vyetu na kujipikia wenyewe kutokana na chakula tulichokuwa tukikipata kutoka hospitali ya mkoa kusitishwa bila ya kuambiwa sababu ya kufanya hivyo.
“Hapa tupo zaidi ya 100 kutoka wilaya mbalimbali za Mkoa wa Dodoma wengine tunalazimika kulala chini vitanda havitoshi, vyoo vyevyewe matundu yapo mawili na mabafu mawili yaani tukianza kuoga ni foleni na kwenda msalani ni foleni,” Rose.
Akijibu malalamiko hayo, Muuguzi wa zamu katika hospitali hiyo, Sista Cesilia Sanya, aliwaahidi akinamama hao kuwa suala la walinzi kutofungua geti halitajirudia.
Hata hivyo, alisema hospitali imepokea malalamiko ya akina mama hao na walinzi waliobainika kufanya vitendo hivyo watachukuliwa hatua.
MWANANCHI
Maiti 13 kati ya 19 za watu waliopoteza maisha katika ajali ya Basi la Nganga Express na lori iliyotokea juzi eneo la Iyovi, Milima ya Udzungwa mkoani Morogoro wamezikwa jana katika kaburi la pamoja eneo la Msamvu mkoani hapa.
Simanzi na vilio vilitawala katika eneo hilo wakati miili ya watu hao ilipofikishwa hapo saa saba mchana kabla ya mazishi hayo kuanza ya saa 8.30 mchana.
Viongozi wa dini zote walifanya misa za kuwaombea marehemu hao waliopoteza maisha katika ajali hiyo ambayo baada ya kutokea, basi na lori hilo aina ya Fuso yaliteketea kwa moto na abiria waliokuwamo.
Akizungumza katika mazishi hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, John Henjewele alisema tukio hilo ni la kusikitisha na la tofauti ambalo limeitia simanzi nchi nzima.
“Ni tukio la nadra sana, lakini pia naweza kusema ni la kizembe kwa sababu tayari tumejua chanzo cha ajali hiyo,” .
Henjewele alisema wamepata malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu madereva wanaoendesha magari ovyo.
“Nawapongeza vijana wa eneo hili kwa kusaidia kutoa miili kwenye magari licha ya kuwa moto ulikuwa unawaka,” alisema Henjewele katika mazishi hayo yaliyohudhuriwa pia na Kiongozi wa ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe.
Miili ya abiria wengine sita, imetambuliwa na ndugu zao ilikohifadhiwa katika Hospitali ya Mtakatifu Kizito, Mikumi Wilaya ya Kilosa.
MTANZANIA
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limekiri kupokea barua iliyotolewa na mawakili wa Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ya kulitaka kuonyesha kifungu cha sheria kinachomtaka mtu kutoa hati ya mali anazozimiliki.
Hata hivyo, jeshi hilo limekataa kuzungumzia chochote kuhusu barua hiyo, lakini limeahidi kuijibu baada ya kuwasiliana na mpelelezi wa kesi hiyo na mwanasheria wa Serikali.
Akizungumza jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, alisema barua imeshapokewa, lakini hawezi kuijibu kwa haraka.
“Siwezi kujibu barua hiyo kwa sasa, tutakapokaa na kujadili ndipo tutakapopata jibu la kutoa juu ya barua hiyo.
“Haya mambo yote yanaenda kisheria, hivyo tunatakiwa tukutane na mpelelezi wa kanda pamoja na mwanasheria wa Serikali muda wowote kuanzia sasa ili tuijadili barua hiyo na kuweza kuipatia majibu,” Kova.
Aprili 16, mwaka huu, Jeshi la Polisi lilimtaka Askofu Gwajima kupeleka nyaraka 10 za mali anazomiliki ikiwamo helkopta baada ya kumaliza mahojiano yao yaliyofanyika Aprili 9.
Nyaraka hizo ni pamoja na hati ya usajili wa kanisa, bodi ya baraza la wadhamini wa kanisa, idadi ya makanisa anayomiliki pamoja na matawi yake.
Nyingine ni za muundo wa utawala wa kanisa, waraka wa maaskofu, hati za kanisa, nyumba na mali za kanisa pamoja na mpigapicha za video za kanisa.
Machi 26, mwaka huu, Askofu Gwajima alijisalimisha katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam baada ya kutakiwa na jeshi hilo kufanya hivyo kwa tuhuma za kumkashifu Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo.
MTANZANIA
Serikali imeshindwa kuweka wazi kufungwa kwa shule zake za sekondari kutokana na ukosefu wa chakula unaozikabili.
Badala yake imewatupia lawama wakuu wa shule zilizoamua kuwarudisha wanafunzi makwao kutokana na kukosa chakula cha kuwalisha.
Baadhi ya shule za sekondari nchini hivi karibuni zilifungwa kutokana na kukabiliwa na uhaba wa chakula baada ya wazabuni kugoma kuwasambazia chakula kwa sababu hawajalipwa fedha zao kwa muda mrefu.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Jumannne Sagini alisema mkuu wa shule mwenye mamlaka ya kufunga shule hizo ni Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Alisema Serikali hutoa huduma ya chakula kwa shule za sekondari za bweni na shule za msingi elimu maalum za bweni kwa kuzingatia fedha zilizotengwa na upatikanaji wake katika mwaka husika.
Alisema fedha za chakula hutolewa kwa awamu na kukamilishwa katika kipindi cha mwaka wa fedha unaotekelezwa.
“Kati ya Julai 2014 hadi Machi 2015, Serikali imetoa Sh bilioni 28.1 kwa ajili ya chakula cha wanafunzi ambazo ni sawa na asilimia 66.7 ya Sh bilioni 42.1 zilizotengwa kwa mwaka 2014/15,Kiasi kilichobaki ni Sh bilioni 13.9 sawa na asilimia 33.23 ya fedha zilizotengwa,”alisema.
Sagini alisema kiasi hicho cha fedha hupelekwa katika hamashauri na baadaye wazabuni hulipwa kwa kuzingatia huduma waliyotoa kwa kila shule.
“Shule nyingi zilikuwa katika kipindi cha mapumziko mafupi kati ya Machi 28, hadi Aprili 14, mwaka huu… katika kipindi hiki wanafunzi walitakiwa kwenda nyumbani kwa ajili ya mapumziko na shule nyingi zimefungua April 8, mwaka huu na nyingine April 12, hivyo wanafunzi walikuwa nyumbani katika mapumziko mafupi ya kawaida,” alisema.
MTANZANIA
Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, aliugeuza Mkoa wa Morogoro kuwa wa viwanda lakini kushindwa kusimamiwa kwa sera zake na viongozi wa Serikali iliyoko madarakani kumesababisha wananchi wake kubaki maskini.
Kauli hiyo aliitoa jana mjini hapa alipohutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Ndege mjini hapa.
Alisema ndiyo maana ACT- Wazalendo inaamini katika misingi ya Nyerere inayoleta usawa wa kidemokrasia na kuimarisha uchumi wa kila Mtanzania.
“Mwalimu Nyerere aliipenda Morogoro kwa kuigeuza kuwa mkoa wa viwanda lakini leo hii viwanda vya sukari asilimia 50 hapa na hakuna kiwanda kipya cha sukari tofauti na alivyovijenga Mwalimu.
“Mtibwa, Kilombero, Kagera na TPC Moshi vyote vilijengwa enzi za mwalimu, lakini leo hii viwanda vinapata ushindani mkubwa kutokana na uagizaji wa sukari kutoka nje ya nchi na hata kuzuiwa viwanda vipya kujengwa,” Zitto.
Alisema pamoja na kujengwa viwanda hivyo bado vimekuwa vikiwanyonya wakulima wa miwa na hivyo kusababisha kilimo chao kutofaidisha wakulima wa miwa kama inavyofanyika kwenye bei na hawana haki ya kujua thamani ya miwa yao.
Kutokana na hali hiyo alisema chama cha ACT-Wazalendo kinataka kupiga marufuku uagizaji wa sukari bila kodi, huku akishauri kuanzishwa kwa viwanda vidogo vya miwa na wananchi wanaolima miwa wote kuwa na hifadhi ya jamii kuweza kuboresha maisha yao ya sasa na baadaye.
Zitto ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema Mkoa wa Morogoro unazalisha nusu ya sukari nchini.
“Hata hivyo sukari nchini haitoshi kwani uwezo wetu ni kuzalisha tani 300,000 wakati mahitaji ni tani 500,000. Ili kuhakikisha bei ya sukari inakuwa himilivu ACT inapendekeza viwanda vya sukari kupewa bei nafuu ya umeme kama ruzuku,” alisema.
Akizungumzia jinsi Mkoa wa Morogoro unavyochangia katika Pato la Taifa (GDP), Zitto alisema unashika nafasi ya sita kati ya mikoa 21 ya Tanzania Bara lakini bado upo chini kwa maendeleo.
HABARILEO
Rais Jakaya Kikwete amesema hajaletewa majina ya watu 16 waliohukumiwa kifo kutokana na mauaji ya maalbino nchini kwa sababu safari ya kisheria ya majina hayo kufikishwa kwake ni ndefu.
Aliyasema hayo juzi wakati alipozungumza katika ibada maalumu ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Askofu Liberatus Sangu kuwa Askofu wa Jimbo la Kanisa Katoliki la Shinyanga.
Akizungumza katika ibada hiyo iliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Mama Mwenye Huruma, Ngokolo, mjini Shinyanga na mbele ya viongozi wengi wa Kanisa hilo wakiwemo maaskofu wakuu, maaskofu na maaskofu wasaidizi 38, Rais Kikwete alitumia nafasi hiyo kujibu madai kuwa Serikali yake haichukui hatua za kutosha kukabiliana na mauaji ya albino.
Pia kufafanua juu ya shinikizo ambalo linatolewa na baadhi ya mashirika yasiyokuwa ya serikali yakimtaka Rais kutia saini ya kuruhusu watu hao wanyongwe.
“Naomba mtusaidie kuielimisha jamii ili iachane na imani za kishirikina, Vikongwe wanauawa kwa sababu tu ya kuwa na macho mekundu na ujinga uliokithiri unaosababisha Watanzania wenzetu wenye ulemavu wa ngozi (albino) kusakwa na kuuawa kikatili kabisa.”
“Nawaombeni sana viongozi wa dini tusaidiane katika kukomesha ujinga huu mkubwa kwa kutoa elimu kwa waumini wenu, ili wajue kuwa vikongwe wana macho mekundu kwa sababu ya kutumia samadi ya ng’ombe kupikia kwa muda mrefu na kuwa kiungo cha albino hakiweza kuleta utajiri wowote,” Rais aliwaambia viongozi hao wa dini.
Kuhusu madai kuwa Serikali yake haichukui hatua za kutosha kukabiliana na mauaji ya albino, Rais Kikwete aliwaambia viongozi hao:
Watu 16 tayari wamehukumiwa kifo na wengine wanasubiri…kesi zao zinaendelea kusikilizwa. Yapo maneno maneno, lakini binafsi kama Rais sijaletewa majina ya watu hao.” Aliongeza:
“Ni lazima tuelewe jinsi mfumo wetu wa kutoa haki unavyofanya kazi hasa katika eneo hilo la kunyonga ama kutokunyonga.
Ni mlolongo mrefu. Katika kesi za watu kuhukumiwa kifo, kwanza kukata rufani ni lazima na wala siyo jambo la hiari ama matakwa ya aliyehukumiwa.
HABARILEO
Serikali imesema ajira za walimu wapya zitaanza rasmi Mei Mosi, mwaka huu huku ikiweka wazi kuwa walimu hao wasitegemee kupangiwa katika maeneo ya majiji, manispaa na miji.
Walimu hao wametakiwa kutotegemea kupangiwa katika maeneo hayo kutokana na idadi ya walimu waliopo ni kubwa na inakidhi mahitaji, huku maeneo yaliyopewa kipaumbele ni vijijini na halmashauri ambazo zina mahitaji na upungufu mkubwa wa walimu.
Idadi ya walimu wapya watakaoanza ajira zao mwezi ujao ni 31,056 ambapo kwa walimu wa ngazi ya Cheti ni 11,795, Stashahada (Diploma) 6,596 na wenye Shahada (Degree) 12,665.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Jumanne Sagini wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ajira mpya za walimu kwa mwaka 2014/2015.
Alisema kwa mwaka huu ajira hizo zimechelewa kutokana na TAMISEMI pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kufanya ufuatiliaji wa kina hadi katika ngazi ya shule ili kubaini kwa uhakika mahitaji halisi ya walimu kwa kila halmahauri na shule.
“Ufuatiliaji huo umebaini kuwepo kwa halmashauri na shule hasa za mjini zenye walimu wa ziada na zingine hasa za vijijini zina upungufu mkubwa wa walimu,” Sagini.
Alisema taarifa hizo zimesaidia kuwapanga walimu wapya kwa usawa ili kuondoa uwiano usioridhisha kwenye maeneo mengi ya vijijini.
Alisema kwa sasa wanakamilisha taratibu za kupata kibali kwa ajili ya ajira za walimu na fedha za kuwalipa stahili zao ili waanze ajira zao rasmi mwezi ujao.
Aidha, alisema orodha ya walimu na vituo watakavyopangiwa vitawekwa katika tovuti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI ambayo ni www.pmoralg.com na ya Wizara ya Elimu www.moe. go.tz ifikapo Aprili 24, mwaka huu.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Zuberi Samataba alisema, pia ufuatiliaji huo ulikuwa ni kuhakikisha wanakuwa na taarifa sahihi za walimu wanaoajiri wote ni wapya ambao hawajawahi kuajiriwa ili kuepuka usumbufu kwa walimu ambao hawatoi taarifa.
Alisema baadhi ya walimu ambao wameshaajiriwa wanapoenda kusoma, hupangiwa upya vituo na hawatoi taarifa hivyo kuleta usumbufu wa kuchelewa kutopata mishahara yao.
HABARILEO
Kutokana na mgomo wa madereva wa mabasi ya abiria nchi nzima uliofanyika Ijumaa iliyopita, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilikuwa limeshaandaa mabasi 300 ambayo yangetumika kusafirisha abiria, imebainika.
Chanzo cha habari kutoka serikalini kimebainisha kuwa JWTZ ilikuwa imeweka tayari mabasi hayo na kuwa walikuwa wakisubiri taratibu za kufanya kazi hiyo, ikiwa ni pamoja na kujua safari za mabasi hayo na nauli ambayo wangewatoza wananchi.
Taarifa za ndani zinabainisha kuwa mgomo wa madereva wa abiria ulipangwa kufanyika kwa zaidi ya siku mbili, jambo ambalo lilifanya serikali kuliandaa jeshi kuwa tayari kutoa huduma kwa wananchi.
Ijumaa iliyopita, mamia ya abiria katika maeneo mengi ya nchi walipata madhila na mahangaiko baada ya madereva wa mabasi ya abiria nchi nzima kugoma, wakishinikiza serikali kubadili masharti ya kutakiwa kusoma kila wanaposajili leseni zao za udereva kila baada ya miaka mitatu, na matumizi ya tochi barabarani unaofanywa na askari wa usalama barabarani.
“Mbali na kulinda mipaka ya nchi kutoka kwa maadui wa nje, jeshi pia lina wajibu wa kuimarisha amani na usalama, na pia kufanya shughuli za kijamii kama vile kuingilia na kutoa huduma fulani muda wowote wanapotakiwa kufanya hivyo na serikali,” ilibainika.
Huu ni ushahidi kwani JWTZ imekuwa ikishiriki kusaidia jamii katika masuala mbalimbali wanapohitajika, ikiwa ni pamoja na kutumia vifaa vyao kujenga madaraja ya dharura, kuokoa maisha ya watu na kutolea mfano wa mafuriko ya Jangwani mwaka 2011 ambapo Jeshi lilishiriki katika kuwaokoa watu waliokuwa wamekwamba kwenye nyumba zilizokuwa zimezingirwa na maji.
Chanzo cha habari kimebainisha kuwa Jeshi lina mabasi mengi, na kutoa mfano tukio la hivi karibuni nchini Malawi wakati Rais Peter Mutharika alipotangaza hali ya hatari, JWTZ ilitoa malori 46 yaliyotumika kusafirisha msaada wa mahindi na dawa kwenda Malawi.
Kwa mujibu wa Nyasa Times, Serikali ya Tanzania ilichangia tani 1,200 za mahindi na dawa za binadamu katika kuisaidia serikali ya Malawi kupunguza uhaba wa chakula na magonjwa miongoni mwa maelfu ya Wamalawi kutokana na mafuriko ambayo yaliikumba nchi hiyo.
millardayo.com ndio sehemu yako kuzipata story zote mtu wangu, unaweza kuwa karibu zaidi na mimi kwa kujiunga kwenye Facebook, Twitter na Instagram pia zitakufikia zote mtu wangu, jiunge hapa >>>twitter Insta Facebook