Kocha wa Manchester United Louis Van Gaal amezoeleka kuwa aina ya kocha ambaye hapendi masikhara toka kwa wachezaji wake na amekuwa si mzito kufanya maamuzi ya kumuondoa mtu kwenye timu pale ambapo anaona anakwenda kinyume na matarajio yake .
Hilo lilidhihirika siku chache zilizopita wakati ambapo kocha huyo alipotangaza wazi kuwa na mpango wa kumuuza kipa namba mbili Victor Valdez kutokana na kushindwa kuendana na falsafa zake .
Van Gaal alisema wazi kuwa Valdez hana maisha ndani ya United kwa sababu alionyesha kwenda kinyume na maelekezo ya kocha wake wakati alipokataa kucheza mechi za kikosi cha wachezaji wa akiba .
Valdez alijiunga na Manchester United baada ya kuwa nje ya uwanja kwa muda wa zaidi ya miezi sita akiwa anauguza jeraha la goti na Van Gaal alimpa nafasi ya kuonyesha uwezo wake ndani ya United msimu uliopita .
Waandishi wa habari walimhoji Van Gaal kwanini Valdez hajaambatana na wachezaji wenzie kwenye ziara ya klabu hiyo nchini Marekani na jibu la kocha huyo lilikuwa jepesi , kipa huyo hana nafasi kwa kuwa ameonyesha ukaidi .
Kwa sasa United bado iko kwenye harakati za kusaka kipa namba moja kufuatia mpango uliopo wa kipa wake namba David De Gea kujiunga na Real Madrid .