MWANANCHI
Kasi ya ukuaji wa uchumi nchini imeshuka kwa asilimia 2.1 katika robo ya kwanza ya mwaka huu.
Hali hiyo inaelezwa kuchangiwa na kushuka kwa uzalishaji katika sekta za madini, mazao ya chakula, habari na mawasiliano.
Wataalamu wa uchumi wanaeleza kuwa uchumi utaendelea kushuka zaidi kutokana na athari za Uchaguzi Mkuu na mpango wa Serikali wa kubana matumizi yake.
Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa la Takwimu (NBS), Morrice Oyuke alisema jana kuwa kasi ya Ukuaji wa Pato la Taifa (GDP), imeshuka kutoka asilimia 8.6 2014 hadi kufikia asilimia 6.5 katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu.
Alisema sekta ya madini imefanya vibaya zaidi kutokana na rekodi ya kukua kwa kasi ya asilimia 0.6 katika kipindi hicho, ukilinganisha na ukuaji wa asilimia 19.7 mwaka 2014.
“Sekta ya madini haijafanya vizuri kutokana na kushuka kwa bei ya madini katika soko la dunia, lakini uzalishaji katika baadhi ya migodi kama Tulawaka umepungua,” alisema.
Oyuke alisema ukuaji wa sekta za kilimo na mifugo umeshuka kutoka asilimia 3.4 mwaka 2014 hadi asilimia 2.6 kutokana na ukame katika maeneo mengi nchini na kuathiri uzalishaji wa mazao.
Hata hivyo, alisema ukuaji wa uchumi umechangiwa kwa kiasi kikubwa na mafanikio makubwa ya uzalishaji wa nishati ya umeme na maji uliokuwa kwa asilimia 0.6.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti ya Repoa, Prof. Samuel Wangwe alisema kasi ya ukuaji wa uchumi itaendelea kushuka kutokana na Serikali kuminya matumizi katika taasisi zake ambazo huwa ndiyo chachu ya kuukuza.
MWANANCHI
Jeshi la Polisi, jana liliuzuia msafara wa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa kwenda Usangi, wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro kushiriki mazishi ya kada wa CCM, Peter Kisumo, likitaka kupunguzwa kwa idadi ya watu.
Mbali na kuzuia msafara huo, chombo hicho cha Dola kimepiga marufuku shughuli za kutafuta udhamini kwa wagombea urais wa vyama vya siasa kuambatana na misafara.
Lowassa, ambaye aliwasili Kilimanjaro jana asubuhi kabla ya kuanza safari ya kwenda Mwanga, alijikuta akikumbana na kizuizi cha polisi walioziba barabara kwa magari yao eneo la Kijiji cha Mroro, mita chache kutoka Mji wa Mwanga, wakati akielekea na msafara wake katika Tarafa ya Usangi kuhudhuria mazishi ya mwanasiasa huyo mkongwe aliyefariki wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.
Lowassa hakukubaliana na agizo la polisi la kumruhusu aendelee na safari na kuwaacha wafuasi wake kwenye msafara huo, ambao awali walitakiwa wasibebe bendera, lakini baadaye wakazuiwa.
Kisumo alizikwa jana katika mazishi yaliyohudhuriwa na maelfu ya waombolezaji, wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete.
“Kwa kuwa tumezuiwa na polisi, kitendo hiki kimeondoa mwafaka wa kitaifa kwamba mpinzani hawezi kumzika mtu wa CCM na wa CCM hawezi kumzika mpinzani…. mpasuko huu ni mkubwa. Wameyataka wao,” alisema Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia baada ya polisi kuwazuia.
“Kwa kuwa wametuzuia kwenda kumzika Mzee Kisumo, sisi tunarudi lakini Watanzania wapewe taarifa kuwa CCM inalipasua Taifa.”
Alipoulizwa sababu za polisi kuwazuia, Mbatia alisema: “Wanahofia Mheshimiwa Lowassa na msafara wake. Magari mangapi? Magari 10 tu ya Mheshimiwa Lowassa! Magari gani hayo?”
Msafara huo ulikuwa na viongozi mbalimbali wa vyama vya upinzani ambao ni pamoja na Mbunge wa Moshi Mjini, Phillemon Ndesamburo, Joseph Selasini (Rombo), Mbatia na Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo pamoja na viongozi wa Chadema ngazi ya mkoa na wilaya.
Msafara huo ulipofika Mroro, ulikutana na kizuizi cha polisi pamoja na askari wa kuzuia ghasia waliowataka watoe bendera na kuachana na msafara huo.
Kutokana na kauli hiyo, Mbatia, ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) aliwataka madereva wa bodaboda kutoa bendera zao na kutoongozana na msafara, agizo ambalo walilitii na kuondoka lakini polisi walikataa magari kuvuka kizuizi hicho.
Baadaye, Mbatia alizungumza kwa simu na Inspekta Jenerali wa Polisi, Ernest Mangu kabla ya kumpelekea simu Lowassa ambaye naye alizungumza naye na kusema wameruhusiwa, lakini askari waliokuwa wameweka doria walikataa kuwaruhusu.
Kutokana na hali hiyo, Mbatia baadaye alizungumza kwa simu na kudai anawasiliana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Fulgence Mponji lakini askari waliokuwapo walidai kuwa wamepewa maagizo kuzuia msafara huo.
Msafara huo ulikaa eneo hilo zaidi ya saa mbili na baadaye polisi waliruhusu gari ya Lowassa, Mbatia na Ndesamburo kupita, lakini watu waliokuwa kwenye msafara wabaki kitendo ambacho viongozi hao walikipinga na kuamua kurudi Moshi.
“Tumeongea na IGP, RPC lakini tunaambiwa OCD amekataa, tunataka Watanzania wajue kuwa CCM wameanza kupasua amani ya Taifa hili,” Mbatia.
Baada ya kukubaliana, Mbatia aliwataka wananchi waliokuwa wanakwenda kwenye msiba kwa msafara wao kuingia kwenye magari na kuanza safari ya kurejea Moshi na baada ya kufika Njia Panda Himo, walikutana na wananchi wengi waliokuwa wakitaka kumuona Lowassa na kufunga barabara.
Polisi walilazimika kutumia bomu la machozi kuwatawanya, lakini wengi waligoma kuondoka na Lowassa alilazimika kusimama kwenye gari na kuwapungia ndipo walipokubali kusogea pembeni kupisha msafara uendelee na safari.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Kamanda Mponji alikiri jeshi lake kuzuia msafara huo, akisema kazi yake ni kuhakikisha Rais anamaliza safari yake Kilimanjaro kwa amani.
Mazishi ya mwanasiasa huyo mkongwe yalitarajiwa kumkutanisha Lowassa na Rais Kikwete, marafiki wawili wa muda mrefu ambao katika siku za karibuni wanaonekana kutofautiana baada ya jina la waziri huyo mkuu wa zamani kuenguliwa kwenye mchakato wa urais kwa tiketi ya CCM mapema Julai.
Lowassa, ambaye amepitishwa na Chadema kugombea urais na ambaye ataungwa mkono na vyama vinne vya NCCR-Mageuzi, NLD, Chadema na CUF, anatarajiwa kuanza kusaka wadhamini leo mkoani Mbeya na baadaye ataelekea Mwanza.
MWANANCHI
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja na aliyekuwa mwenyekiti mkoa wa Dar es Salaam John Guninita wametangaza leo kuachana na CCM na kujiunga Chadema.
Makada hao wa CCM wametangaza kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Dar es Salaam leo.
Wakizungumza katika mkutano huo, makada hao wamesema wamechukua uamuzi huo baada ya kubaini CCM imepoteza mwelekeo na kwamba kinaendeshwa kibabe tofauti na misingi ya kuasisiwa kwake.
Wametolea mfano wa kukiukwa kwa demokrasia kulikofanywa wakati wa mchakato wa kutafuta mgombea urais wa chama hicho ambapo Dr John Magufuli aliteuliwa kupeperusha bendera ya CCM.
Hatua ya makada hao imekuja ikiwa ni siku moja tu tangu aliyekuwa mbunge wa chama hicho jimbo la Sikonge, Said Nkumba atangaze kuachana na chama hicho na kujiunga na Chadema.
Huo ni mwendelezo wa matukio ya makada na wabunge chama hicho kuhamia upinzani hasa Chadema kwani awali aliyekuwa waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa aliachana na CCM baada ya jina lake kukatwa na kamati ya maadili ya chama hicho.
Wengine waliohama CCM ni aliyekuwa mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck Ole Medeye, aliyekuwa mbunge wa Segerea, Makongoro Mahanga ambaye pia ni naibu waziri Kazi na Ajira, aliyekuwa mbunge wa Kahama, James Lembeli, aliyekuwa mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM, Mgana Msindai na mbunge wa viti maalumu anayemaliza muda wake Esther Bulaya.
MWANANCHI
Maziko ya mwanasiasa mkongwe nchini, Peter Kisumo yametawaliwa na siasa za ‘chini chini’ kati ya makada wa CCM na wanachama wa Chadema huku Rais Jakaya Kikwete akishindwa kutoa hotuba.
Badala yake, salamu za Rais ambaye alikuwa rafiki wa karibu na marehemu zilitolewa kwa niaba yake na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha Rose Migiro.
Tukio jingine lililozua gumzo ni la makada wa CCM, wakiwamo viongozi waandamizi wa chama hicho kushiriki katika tukio la kumpokea Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa katika Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (Kia).
Hata hivyo, makada hao ambao ni Katibu wa Uchumi wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Paul Matemu na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM )wa mkoani hapa, Fred Mushi hawakufika kwenye maziko hayo yaliyofanyika Usangi.
Makada hao walikuwa katika msafara wa Lowassa ulioishia Mwanga baada ya kudhibitiwa na polisi.
Matemu alipoulizwa na kama ushiriki wake katika mapokezi ya Lowassa hauwezi kumletea matatizo, alisema siasa siyo uadui au uhasama na kwamba msiba hauna itikadi.
“Hivi tunapokwenda msibani ni marufuku wafuasi wa vyama viwili kupeana lifti au kwenda pamoja? Hivi nchi hii ndiyo imefika huko? Tukianza kubaguana kwenye misiba ni hatari,” Matemu.
Awali, msafara wa Rais Kikwete uliwasili katika Uwanja wa Taifa ulio jirani na Kanisa Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kivindu, Usangi saa 9.20 alasiri kwa helkopta mbili zilizowasili kwa kupishana kwa dakika 12.
Akitoa salamu za Rais, Dk Migiro alisema Taifa linajivunia maisha ya Kisumo kwani alikuwa na msimamo thabiti katika masuala mbalimbali ya kitaifa.
“Aliyafanya hayo akilenga kuimarisha misingi ya utawala bora na alishiriki pia kutoa ufafanuzi wa kimantiki katika masuala mbalimbali wakati wa kuandika Katiba Mpya,” Dk Migiro.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya familia ya Kisumo, Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya aliishukuru Serikali na Rais Kikwete kwa kugharimia matibabu ya Kisumo.
MWANANCHI
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahimu Lipumba alirejea nchini jana jioni akitokea Kigali, Rwanda alikokwenda mara tu baada ya kujiuzulu wadhifa huo siku nane zilizopita.
Profesa Lipumba aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) saa 10.10 jioni kwa ndege ya Rwanda Air.
Akihojiwa na Azam Tv kwa simu akiwa Kigali, siku tatu baada ya kuondoka nchini, Profesa Lipumba alisema alikuwa nchini humo akifanya utafiti kuona namna gani Tanzania inaweza kujifunza mambo ya kiuchumi kutokana na nchi hiyo kupiga hatua kubwa katika sekta hiyo.
Alipoulizwa jana, Profesa Lipumba alisema akiwa huko alikuwa na mazungumzo na Bodi ya Maendeleo ya Rwanda (RDB), wadau wa masuala ya rushwa, waziri wa fedha wa nchi hiyo na makamu mwenyekiti wa Bodi ya Utawala.
“Wenzetu wamepiga hatua kubwa katika kukuza uchumi ndani ya kipindi kifupi, hivyo safari yangu ilikuwa ya kujifunza mbinu walizotumia kufikia malengo yao,” alisema.
Akizungumzia hatima yake kisiasa, licha ya kusema ataendelea kuwa mwanachama wa CUF, alisema hatashiriki kufanya kampeni kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kwa kuwa umoja huo umemsimamisha mwanachana wa CCM, Edward Lowassa.
“Kisiasa hatima yangu ni kama ya Mtanzania mwingine yeyote, Ukawa tuna mgombea kutoka CCM, amehama juzi tu, pia mle ndani ya Bunge la Katiba hakuunga mkongo Rasimu ya Katiba na ndiyo maana nikasema dhamira yangu inanisuta,” Lipumba.
Alisema wanachama wa CUF hawana sababu ya kuona kama amewaacha kwa kuwa bado yupo nchini.
Awali, akitangaza kujiuzulu, nguli huyo wa uchumi, alisema alifikia uamuzi huo kutokana na Ukawa kumkaribisha Lowassa kugombea urais kupitia umoja huo, hivyo dhamira yake inamsuta.
NIPASHE
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amefunguka kwa mara ya kwanza na kuweka wazi kilichotokea mjini Dodoma na kusababisha ashindwe katika uteuzi wa kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Membe amekuwa kada wa tatu kueleza hadharani jinsi uteuzi huo ulivyoendeshwa ambao Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, aliibuka kidedea kati ya makada 42 waliojitokeza kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa.
Makada wengine waliojitokeza hadharani kuelezea mchakato huo ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya, ambao kwa nyakati tofauti walieleza sababu mbalimbali zilizosababisha kushindwa kwao.
Membe akizungumza jijini Dar es Salaam jana katika kongamano la pili la Watanzania waishio ughaibuni (Diaspora), alisema mchakato huo ulikuwa ni sawa na timu mbili za mpira wa miguu zilizokuwa zinapambana uwanjani.
Alisema unaweza ukapata timu nzuri sana ya mpira kwenye ligi na ikashinda michezo yote bila kufungwa goli hata moja.
Aliongeza kuwa lakini mwishoni timu hiyo inapotoka sare na timu nyingine ambayo ni dhaifu kwenye fainali, timu hizo zinakwenda kwenye penalti kwa kuwa mshindi lazima apatikane.
Membe alieleza kuwa wakati wa upigaji penalti timu hiyo ambayo ilitarajiwa kuibuka na ushindi kwa kuwa ilicheza mpira safi ikafungwa penalti zote tano na hiyo timu ambayo haikutegemewa ikashinda mabao yote.
Alisema kuwa kwenye ‘football jargon’ kitendo hicho cha timu iliyocheza mpira vizuri na kudhaniwa ingeibuka na ushindi, lakini ikashindwa kwenye penalti, timu hiyo imekufa kifo cha ghafla.
Membe aliendelea kueleza kuwa timu hiyo itakuwa imepigwa kifo cha ghafla na kueleza kuwa inapopigwa kifo cha namna hiyo timu hiyo haiwezi kutegemewa isimame na ielezee kilichotokea.
“Naomba leo nitumie nafasi hii kwa mara ya kwanza kuelezea kilichotokea mjini Dodoma katika uchaguzi wa nafasi ya urais kwa Chama Cha Mapinduzi na nadhani sitaulizwa tena,” alisema Membe.
Mfano huo huenda ukahusishwa na wanachama wa CCM waliokuwa wanamuunga mkono Membe kama timu iliyokuwa inatumainiwa ingeshinda mchakato huo, huku Dk. Magufuli akielezwa kama timu ambayo haikudhaniwa kushinda kinyang’anyiro hicho kutokana na kutokuwa na makundi yaliyokuwa yanamuunga mkono.
Membe alikuwa na kundi kubwa la wafuasi akimfuatia Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Lowassa na Membe walikuwa miongoni mwa makada sita ambao walipewa adhabu ya kufungiwa mwaka mmoja kuanzia Februari, mwaka jana hadi Mei, mwaka huu, baada ya kubainika kuwa walianza kampeni mapema kabla ya wakati kinyume cha kanuni za chama hicho.
HABARILEO
Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imekipa onyo kituo cha utangazaji cha Independent Television (ITV) kutokana na kutangaza taarifa zisizo za kweli na za uchochezi.
Aidha, imevitaka vituo vya utangazaji nchini kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ili kuzuia uvujifu wa amani na kuwa hawatasita kuchukua hatua kali kwa watakaokiuka taratibu hizo.
Akisoma hukumu dhidi ya ITV, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Margaret Munyagi alisema kituo hicho katika kipindi cha ‘Habari zilizotufikia hivi punde’, kati ya saa 2:00 na saa 5:00 asubuhi, Agosti 10 mwaka huu, kilitangaza taarifa ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kupiga marufuku maandamano ya mgombea urais kupitia Umoja wa Vyama vinne vya upinzani (Ukawa) Edward Lowassa.
“Mtangazaji pia alisikika akisema habari zilizoifikia ITV na Radio One, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limepiga marufuku maandamano ya Chadema kupitia Ukawa kwenda kuchukua fomu ofisi za Tume,” alisema.
Munyagi alisema baada ya kuridhika na ushahidi wa video ya taarifa hiyo na kupokea utetezi kutoka kwa uongozi wa ITV na Radio One, Kamati imekipa onyo kali kituo hicho na kutakiwa kukanusha habari hizo katika kipindi cha taarifa ya habari ya saa 2:00 asubuhi na usiku kwa siku mbili mfululizo.
“Endapo ITV watakiuka kutekeleza adhabu hiyo, kamati yake haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya kituo hicho. Pia ITV inaweza kukata rufaa ndani ya siku 30 tangu kutolewa kwa hukumu,” alisema.
Awali, katika utetezi wao, uongozi wa ITV na Radio One walisema habari hiyo haikuwa na msingi wa uchochezi bali lilikuwa ni ombi la Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova aliyetaka kukanusha taarifa zilizozagaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa polisi wamezuia maandamano hayo.
Mkurugenzi wa Radio One na ITV, Joyce Mhavile aliomba radhi kwa kosa hilo na kuahidi kuwa watakuwa makini katika taarifa zao.
HABARILEO
Polisi imesitisha maandamano wakati wa uchukuaji au urudishaji fomu pamoja na kutafuta wadhamini mikoani kwa wagombea wa nafasi ya urais na ubunge.
Hatua hiyo imechukuliwa kwa kile kilichoelezwa ni kuweka hali ambayo haitaleta usumbufu au kuhatarisha usalama wa raia na mali zao.
Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahman Kaniki alisema hayo jana jijini Dar es Salaam. Alisema utaratibu wa kuwakutanisha wadau wa siasa ikiwemo viongozi wa vyama vya siasa unaendelea kufanyika kuona namna bora ya kuhakikisha mchakato mzima wa uchaguzi unafanyika katika hali ya amani na utulivu.
“Kwa sababu za kiusalama jeshi linasitisha maandamao ya aina yoyote wakati wa uchukuaji fomu, kutafuta wadhamini mikoani na hata wakati wa kurejesha fomu ili kuweka hali ambayo haitaleta usumbufu au kuhatarisha usalama wa raia na mali zao,” alisisitiza.
Alisema Polisi haitasita kuchukua hatua kwa mgombea, chama au mfuasi yeyote atakayekaidi agizo hilo. Kaniki alisema katika kipindi hiki, baadhi ya wagombea walisindikizwa na wafuasi wao kwenda katika ofisi ya Tume ya Uchaguzi kuchukua fomu na kusababisha ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani na hivyo kuleta usumbufu kwa watumiaji wengine wa barabara.
“Jambo hilo lilisababisha usumbufu na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi walioshindwa kufika kwa wakati katika shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii,” alisema. Alisema wapo ambao walishindwa kuingia maofisini na wengine kukosa huduma za kijamii kutokana na kufungwa kwa maduka.
Alisema pia wapo wagonjwa walishindwa kufika hospitalini kutokana na misafara hiyo mirefu na kwamba usumbufu huo ulitokea wakati wa wagombea wa vyama vya CCM na Chadema walipokwenda kuchukua fomu. Kaniki alisema sababu kubwa za kusitisha maandamano hayo ni za kiusalama baada ya kufanya tathmini.
Alisema kwa mujibu wa katiba, ni haki ya kila mwananchi kuandamana lakini ni lazima kuangalia mwenendo wa maandamano. Alisema haiwezekani shughuli kusimama kwa saa 10 na kuruhusu jambo hilo kuendelea kwa kuwa si kuwatendea haki watu wengine.
HABARILEO
Vituo vya maarifa sita vitakavyotoa huduma za afya vinatarajiwa kujengwa kando ya barabara kunusuru madereva wa masafa marefu kutoka Dar es Salaam hadi Tunduru.
Meneja Mradi wa North Star Alliance anayeratibu ujenzi huo, Edger Mapunda alisema jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Mapunda alisema wanatambua sekta ya usafirishaji inakabiliwa na changamoto ya masuala ya Ukimwi hivyo wameona kuna sababu ya kuwasaidia madereva kwa kuwa wawapo safarini wanakutana na watu mbalimbali. Alisema ujenzi wa vituo hivyo utakapokamilika utawanufaisha pia wananchi waliopo jirani na vituo hivyo.
Pia watatoa elimu ya afya, upimaji wa magonjwa mbalimbali ikiwemo kisukari pamoja na uendeshaji salama kwa madereva wawapo barabarani. Alisema vituo viwili vitajengwa katika jiji la Dar es Salaam eneo la bandarini, vingine viwili vitajengwa katika mkoa wa Iringa na viwili vitajengwa mkoani Mbeya.
“Maambukizi ni makubwa katika maeneo hayo. Tulifanya tafiti tokea mwaka 2013 tukagundua mkusanyiko ni mkubwa katika maeneo hayo. Pia Tunduma na Iringa tuligundua huduma za afya sio nyingi,” alisema.
Alisema gharama za mradi mzima ni dola za Marekani milioni moja, na kwamba vituo kama hivyo vimejengwa pia katika nchi ya Kenya ambapo vipo tisa, Afrika Kusini vipo 12 na Malawi viwili.
Mkurugenzi wa Uraghibishi na Habari Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Jumanne Issango alisema wamekuwa na mkutano wa kujadili uanzishwaji wa mradi wa kujenga vituo sita vya maarifa kandokando ya barabara kuanzia Dar es Salaam hadi Tunduru.
Alisema mradi huo utakuwa wa miaka mitatu ulianza Aprili mwaka huu na kumalizika mwaka 2018. Mwakilishi wa madereva wanaosafiri masafa marefu kutoka Chama cha Madereva nchini, Mohamed Sharrif alisema amekuwa na wasiwasi na mradi kama huo unapomalizika huduma zinazokuwepo zinadumaa kwa kukosa mfadhili.
PAPO KWA PAPO zipate habari zote zinazonifikia za siasa muziki, michezo, maisha, Breaking news na nyingine kwa kujiunga hapa na mimi >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos