Klabu ya Real Madrid imepata pigo kutokana na michezo ya kimataifa iliyokuwa inafanyika kwa muda wa wiki nzima baada ya taarifa za kuumia kwa kiungo wake tegemeo, Luka Modric.
Kiungo huyo ameumia akiwa na timu yake ya taifa ya Croatia katika mchezo dhidi ya Bulgaria ambapo aliumia nyonga na jeraha hili litamuweka nje ya uwanja kwa muda usiopungua wiki tatu.
Modric hata hivyo ana matumaini makubwa ya kurudi uwanjani mapema kiasi cha kuwahi mchezo wa michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Paris St Germain baada ya kukosa michezo takribani mitatu ikiwemo michezo dhidi ya Celta Vigo na Getafe pamoja na mchezo wa kwanza dhidi ya PSG.
Kukosekana kwa Modric kutafungua nafasi kwa viungo wachanga wa klabu hiyo akiwemo Casemiro ambaye amerudishwa msimu huu akitokea Fc Porto na Matteo Kovacic ambaye amesajiliwa msimu huu akitokea Inter Milan.