Ni habari kutoka Mahakamani ambapo upande wa mashtaka umeieleza Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni kuwa jalada la kesi ya wanaodaiwa kumuua bondia maarufu wa Tanzania Thomas Mashali, limepelekwa kwa Mkuu wa Upelelezi (RCO) kwa ajili ya upelelezi.
Hayo yameelezwa na Wakili wa Serikali Yussuf Aboud, mbele ya Hakimu Boniphace Lihamwike wakati kesi hiyo ilipoitishwa kwa ajili ya kutajwa ambapo amedai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
“Jalada la Watuhumiwa kwa sasa limehamishiwa kwa RCO atakapolipitia likikamilika litapelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuendelea na upelelezi,” alisema Wakili Aboud.
Baada ya kueleza hayo Hakimu Lihamwike ameahirisha kesi hiyo hadi November 15, 2017 kwa ajili ya kuendelea kutajwa ambapo Watuhumiwa wote 7 wamerejeshwa Mahabusu.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka Watuhumiwa wanadaiwa kumuua Bondia Mashali, October 31, 2016 huko Kimara Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam ambapo Watuhumiwa wenyewe ni Issa Mwandaka (23), Ramadhan Ally (21), Mohamed Kyamba (22), Charles Manongi (20), Athuman Ramadhan (20), Joseph Maro (19) na Emmanuel Paschal (20).
Ulipitwa na hii? Lulu aliua bila kukusudia – Wazee wa Baraza