Leo March 6, 2018 nakusogezea hukumu iliyotolewa katika Mahakama ya Wilaya Kinondoni ambapo imemhukumu miaka 30 jela mkazi wa Kinondoni Mkwajuni Agnes Mhoja (40), baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kukutwa akisafirisha Kilo 32.57 za dawa za kulevya aina ya Bangi.
Mbali ya Mhoja mshtakiwa mwingine ni Samwel Jangwa (25), ambae aliachiwa huru kutokana na upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha makosa dhidi yake.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Boniface Lihamwike, amesema mshtakiwa Mhoja ametiwa hatiani baada ya mahakama kuridhishwa na ushahidi uliowasilishwa na mashahidi watatu wa upande wa mashtaka.
Amesema ushahidi wa upande wa mashtaka uliotolewa na Ofisa wa ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Mpelelezi na Ofisa wa Polisi aliyemkamata mshtakiwa ulikuwa na vielelezo vya kutosha.
“Kwa mazingira hayo mahakama hii inakutia hatiani kwa kosa hilo kutokana na ushahidi wa kina uliowasilishwa hapa ambao nimeuthibitisha pasi na shaka,” Hakimu Lihamwike.
Hakimu Lihamwike amesema kutokana na mshtakiwa kutiwa hatiani anamuhukumu kwenda jela miaka 30 ambapo hilo litakuwa ni onyo na fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo za kusafirisha Bangi.
Awali Wakili wa serikali, Yussuf Aboud, aliieleza mahakama kuwa hakukuwa na kumbukumbu za makosa ya nyuma dhidi ya mshtakiwa, hivyo mahakama itoe adhabu kali.
Katika utetezi wake, mshtakiwa Mhoja ameiomba mahakama impunguzie adhabu kwa sababu Bangi aliyokamatwa nayo haikuwa mzigo wake halali, pia yeye ni mtu mzima anayetegemewa na familia.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka katika kesi hiyo namba 472/2016 Mhoja anadaiwa akiwa eneo la Kituo cha Mabasi yaendayo mkoani Ubungo, alikutwa akisafirisha Kilo 32.57 za dawa za kulevya (Cannabis Sativa) maarufu kama Bangi.
Inadaiwa ametenda tukio hilo October 30, 2016 eneo hilo la Ubungo ambapo November 15, 2016 alifikishwa mahakamani hapo na kusomewa shtaka lake.
BARUA YA HUSSEIN BASHE KWA BUNGE “UMOJA, USALAMA WA TAIFA”, BONYEZA PLAY HAPA CHINI KUTAZAMA NA KUSIKILIZA