Leo March 7, 2018 taarifa kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu amesema hali ya upatikanaji wa dawa nchini Tanzania imeimarika hadi kufikia asilimia 90.
Akizungumza na waandishi wa habari, Bwanakunu amesema kuna upatikanaji wa dawa muhimu takribani 135.
“Upatikanaji wa dawa hizi muhimu kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ni kati ya asilimia 85 hadi 98, ambapo dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi na malaria ni asilimia 100,” -Bwanakunu
Pia Bwanakunu amesema MSD imetunukiwa Ithibati ya Kimataifa ya Juu ya Ubora inayojulikana kama ISO 90001:2015 ambayo itadumu kwa miaka 3.
“Kampuni ya Kimataifa ya ACM Ltd ilifanya ukaguzi wa ubora wa huduma zinazotolewa na MSD August 2017, ambapo matokea yalithibitisha kuwa huduma tunazotoa za ununuzi, utunzaji na usambazaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara zinafuata miongozo ya Kimataifa,”-Bwanakunu
Mbali na hilo, pia amebainisha kuwa wameanzisha mfuko wenye vifaa vya kujifungulia wakina mama ambao utakuwa na vifaa vyote na utauzwa Shilingi Elfu Kumi na Mbili.