Leo March 22, 2018 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ulinzi wa Israel Avigdor Lieberman Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Mazungumzo yamehudhuriwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Balozi wa Israel hapa nchini Noah Gal Gendler, viongozi wakuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Polisi.
Katika mazungumzo hayo President JPM amemshukuru Lieberman kwa kuitembelea Tanzania na amemhakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ina dhamira ya dhati ya kuukuza zaidi na kuuimarisha uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Israel.
JPM ametaka makubaliano ya ushirikiano kati ya Tanzania na Israel katika maeneo mbalimbali yakiwemo ulinzi na usalama, mafunzo na masuala ya kiuchumi yatiwe saini haraka ili utekelezaji uanze mara moja.
“Tanzania na Israel ni marafiki wa miaka mingi, nataka kuona urafiki wetu unakuwa zaidi, nawakaribisha wawekezaji kutoka Israel kuja kuwekeza katika kilimo, madini na gesi na pia kuwepo ndege za moja kwa moja kutoka Israel hadi Dar es Salaam na Kilimanjaro ili kukuza utalii” -President JPM
President JPM amemuomba Lieberman kumfikishia ujumbe Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wa kumualika kutembelea Tanzania na pia kuanzisha ofisi ya ubalozi hapa nchini badala ya kutumia ofisi za ubalozi zilizopo Nairobi nchini Kenya.
Nae Avigdor Lieberman amemshukuru President JPM kwa kumkaribisha na kufanya nae mazungumzo na pia amemhakikishia kuwa Israel imejipanga kuongeza uhusiano na ushirikiano wake na Tanzania katika maeneo yote ya makubaliano pamoja na kusaidia kilimo na usindikaji wa chakula.
Rais Magufuli amempangia IGP mstaafu Mangu kituo cha kazi