Tosin Olakunle raia wa Nigeria anayejishughulisha na kupamba nyuso za watu na mitindo ya nywele amejikuta akikamatwa na jeshi la polisi kwa kile walichodai kuwa eti ni ‘mwembamba sana halafu ana sura ya kike wakati yeye ni mwanaume’.
Olakunle alijikuta akitoa N2,000 ambayo ni sawa na zaidi ya shilingi 12,647 za kitanzania ili kupatiwa dhamana katika kituo cha polisi cha Iwaya alipokuwa ameshikiliwa na jeshi hilo.
Akielezea mkasa huo Olakunle amesema kuwa ilikuwa jumatatu ya May 28 alipokuwa anaenda kwa mteja wake mmoja kumhudumia na ndipo alipokuwa katika stendi ya Lamata katika mji wa Ojota alipozuiliwa kupanda basi na mtu aliyemtaka ajitambulishe.
“Nilimuuliza kwanini nijitambulishe kwako? Jamaa akanijibu kuwa yeye ni polisi na akanitaka nimpe vitambulisho vyangu kitu ambacho nilitelekeza. Lakini akaniuliza tena kwa nini naonekana kama mwanamke kwenye kitambulisho changu? Nikamjibu kuwa nimekuwa na kitambulisho hicho kwa muda mrefu sasa baadae akaniambia niingie kwenye gari nakuniambia kuwa mimi ni shoga” alisimulia Olakunle.
“Nilimpa simu pamoja na iPad yangu ili akague kuona kama atakuta kitu chochote ambacho kitathibitisha mimi nahusika na vitendo hivyo na nikamwambia kuwa mimi pia ni mwanamitindo wa nywele wala sijapaka vipodozi na wala sina michoro (tattoo) kwenye mwili wangu lakini bado hakunielewa na kuendelea kunishikilia” aliongeza Onlakunle.
Aidha baadae Onlakunle alipelekwa katika kituo cha polisi cha Iwaya na alipouliza kwa nini anashikiliwa na polisi?, askari huyo akamwambia kuwa “wewe ni mwembamba sana na unaonekana kama wewe ni shoga”
Olankunle alimalizia kwa kusema kuwa ilibidi awe mpole ili ajiepushe na kipigo na ikambidi atoe fedha N2,000 na kujidhamini ili aweze kuachiwa huru huku akimkosa mteja wake waliyokuwa wamepanga kukutana.