Leo July 27, 2018 Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Augustino Mrema amemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola awashughulikie waliombambikia kesi ya kumkashfu Rais Mkapa mwaka 1996 kama amedhamiria kuwashughuliki wabambikizaji wa kesi mbalimbali kwa maslahi yao binafsi.
Akizungumza na waandishi wa habari Mrema ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole amesema kama yeye alishika nafasi mbalimbali nchini ameweza kubambikiwa kesi kuwa amemtukana Rais Benjamin Mkapa basi haitashindikana kwa mtanzania wa kawaida kubambikiwa kesi yoyote.
“Watu wanaposema wanabambikiwa kesi sio uongo, nimeamua kuanza na mimi niliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Naibu Waziri Mkuu watu wajue kwamba nilifanyiwa hivi na waliofanya hivi wahojiwe” Mrema
“Jinsi Waziri Kangi Lugola alivyoanza kazi yake amenitia moyo pamoja na watanzania kwa ujumla, naweza nikasema akiendelea hivi anaweza akavaa viatu vyangu,” amesema Mrema
Aidha, amesema Lugola ana kazi kubwa ya kufanya kwasababu Wizara ya Mambo ya Ndani ndio kioo na uchafu wowote unaotaka kuuondosha katika nchi, Wizara hiyo ndio inahusika kwa kiasi kikubwa kutekeleza jukumu hilo.
Amesema yeye kama Mwenyekiti wa Bodi ya Parole bado hajajua ni asilimia ngapi ya waliokuwepo jela wamebambikiwa kesi lakini ni watu wengi.