Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameendelea na ziara yake katika mikoa ya Mwanza na Mara kwa kufungua viwanda 3 vya kampuni ya Lakairo, kuzindua ujenzi wa kiwango cha lami kwa barabara ya Bulamba – Kisorya (51km), kufungua mradi wa maji katika kijiji cha Nebuye kwa ajili ya wananchi wa Nansio.
Viwanda vya kampuni ya Lakairo vilivyopo katika eneo la Isangijo Wilaya ya Magu vinajumuisha kiwanda cha kutengeneza vifungashio vya nafaka, kiwanda cha pipi na jojo na kiwanda cha ‘steelwire’ ambavyo ni uwekezaji wa Mbunge wa Jimbo la Rorya Lameck Airo (Lakairo), uliogharimu Bilioni 20.1 na vimeajiri watu 400.
Akizungumza baada ya kufungua viwanda hivyo Rais Magufuli amempongeza Lameck Airo kwa uwekezaji huo na ametoa wito kwa Mtanzania yeyote mwenye uwezo wa kuwekeza katika viwanda ama biashara kufanya hivyo huku akibainisha kuwa anawapenda wawekezaji na matajiri wanaoendesha shughuli zao kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi.
“Mimi nawapenda wafanyabiashara na matajiri, fanyeni biashara zenu kwa amani lakini zingatieni sheria. Naiagiza Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango kujenga mazingira mazuri ya kuwawezesha wawekezaji hawa hasa hawa wazalendo kama akina Lakairo” amesema Rais Magufuli.