Wakati Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko wakiendelea kusota mahabusu, Wakili anyewatetea Profesa Abdallah Safari amehoji katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuhusu rufaa iliyokatwa na upande wa mashtaka katika Mahakama ya Rufani.
Mbowe na Matiko wanasota mahabusu baada ya Mahakama ya Kisutu kuwafutia dhamana yao November 26,2018 kwa kukiuka masharti ya dhamana, ambapo waliamua kukata rufaa Mahakama Kuu lakini iliwekewa pingamizi baada ya upande wa mashtaka kukata rufaa Mahakama ya Rufani.
Profesa Safari alihoji swali moja kuhusu rufaa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri baada ya Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi kueleza kuwa shauri hilo limeitishwa kwa ajili ya kutajwa.
Baada ya kueleza hayo, Profesa Safari alimuuliza Wakili Kadushi kama rufaa waliyoikata Mahakama ya Rufani ilikuwa chini ya hati ya dharura ama lah na kama haikuwa chini ya hati ya dharura ni kwa nini…?
Katika majibu yake Wakili Kadushi ameeleza kuwa hakuna uhalali wa kisheria kuhusu swali hilo mahakamani hapo, labda lingeulizwa wakiwa Mahakama Kuu ama ya Rufaa.
Kutokana na hatua hiyo, Hakimu Mashauri ameahirisha kesi hiyo hadi January 17,2019 huku akisema swali hilo la rufaa likahojiwe Mahakama Kuu.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Katibu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya na Katibu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu
Wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya February Mosi na 16, mwaka huu maeneo ya Dar es Salaam.