Tunayo stori kutokea Mahakama Kuu ya Tanzania ambapo Septemba 11, 2019 inatarajia kuanza kusikiliza kesi ya mirathi namba 266/2019 iliyofunguliwa na Mary Nyaronga akiomba Mahakama hiyo iwaamuru wasimamizi wa mirathi ya baba yake, John Nyaronga wampatie urithi wake.
Katika kesi hiyo, wasimamizi ambao ndiyo walalamikiwa ni Dk.George Nyaronga, Anna Nyaronga, Bahati Kivugo (mke wa marehemu) na Denis Arego ambaye ni mtoto wa marehemu aliyejitokeza baada ya baba yake kufariki.
Kabla ya Mahakama kupanga kusikiliza kesi hiyo Septemba 11, tayari imeshatoa zuio la kutokuuzwa kwa hoteli ya marehemu Nyaronga ambayo ipo Musoma hadi masuala yaliyokuwepo mahakamani yasikilizwe na kutolewa uamuzi.
Uamuzi wa kuwekwa zuio hilo umetolewa na Jaji Dk. Atuganile Ngwala baada ya kuibuka malumbano baina ya pande mbili wakati kesi hiyo ilipotajwa kwa mara ya kwanza kwa ajili ya kusikilizwa.
Jaji Dk.Ngwala aliwataka upande wa walalamikiwa (wajibu maombi) ndani ya siku 14, kuwasilisha kiapo kinzani mahakamani hapo, ambapo watatakiwa kukiwasilisha Juni 18,2019.
Mary alifungua kesi hiyo kuiomba Mahakama iwaamuru walalamikiwa kumlipa mali za urithi alizogawiwa mara baada ya baba yake kufariki. Anadai kuwa mali hizo hajagawiwa tangu mwaka 2013.
Miongoni mwa mali hizo ni shamba la hekali tatu lililopo Kizito Huonjwa, kijiji cha Kimbiji Beach, shamba namba 2753, lipo Kisanga kijiji cha Kisarawe hekali 14, Injini ya boti iliyopo Chetah, sh milioni 15 kutoka benki ya NMB, Sh milioni 22 kutoka katika hisa za Kampuni ya MSC, shamba hekali 1.2 ambalo lipo Kijiji cha Buganjo.