Rais Magufuli, katika hotuba yake leo Mkoani Mwanza amewapa nafasi Viongozi mbalimbali pamoja na wa Vyama vya Upinzani, akiwemo Freeman Mbowe na Prof. Ibrahim Lipumba kutoa salamu kwa Watanzania.
Akizungumza Mbowe wakati akitoa salamu zake kwa wananchi, amemuomba Rais Magufuli, kutumia siku hiyo kuleta maridhiano yenye mshikamano na upendo, yatakayoleta amani na Demokrasia kwa Taifa.
“Ninamuomba Mwenyezi Mungu siku ya leo ikafungue milango, tuweze kuishi kama Taifa linalopendana, tuvumiliane, tukosoane, turuhusu Demokrasia, tukajenge Taifa lenye upendo na mshikamano na Mh Rais una nafasi ya kipekee kuweka historia ya maridhiano katika Taifa, kwani kuna wengine wanalalamika, wengine wanaumia, kaliweke Taifa katika nafasi ya utengamano” Mbowe.
Kwa upande wa Profesa Lipumba amesema kuwa katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, lipo jukumu la kuhakikisha Demokrasia inakuwepo.
“Natoa pongezi kwa Watanzania wote, kwa kusherehekea miaka 58 ya Uhuru, mimi nilikua naingia darasa la nne, nampongeza Rais kwa kazi aliyoifanya, namuomba ajue anajukumu la kujenga demokrasia kwenye nchi yetu kuelekea Uchaguzi 2020″ Profesa Lipumba.