Waziri Mkuu wa Somalia Hassan Ali Khaire ameondolewa kwenye wadhifa huo katika kura ambayo haikutarajiwa ya kutokuwa na imani naye jana, hatua iliyolitumbukiza Taifa hilo kwenye mzozo wa kikatiba wakati likielekea kwenye uchaguzi mkuu.
Khaire ameipuuzia mbali kura hiyo huku ofisi yake ikisema mchakato huo haukuwa halali, Spika wa Bunge Mohamed Mursal Abdirahman alimshutumu Waziri huyo mkuu aliyeondolewa pamoja na Baraza lake la Mawaziri kwa kushindwa kukamilisha muswada wa katiba ambao ungefungua njia ya kufanyika uchaguzi wa haki.
Hatua hiyo ya kumuondoa ilikuja baada ya mjadala mkali wiki iliyopita kuhusiana na uchaguzi ujao utakavyofanyika, Ubalozi wa Marekani umeelezea wasiwasi wake kufuatia hatua hiyo na kusema ni pigo katika ajenda ya mageuzi ambayo Somalia imekuwa ikiitekeleza kwa msaada wa Marekani.