Afisa wa Shirika moja lisilo la Serikali nchini Niger amesema kuwa kumegunduliwa makaburi sita ya umati yenye maiti za karibu watu 71 wanaodaiwa kuuliwa na Wanajeshi wa Serikali katika eneo la Tillabéri magharibi mwa Niger.
Mwenyekiti wa Shirika lisilo la kiserikali linaloshiriki katika uchunguzi wa Kamisheni ya Taifa ya Haki za Binadamu nchini Niger, Abdullah Sido amesema kuwa baadhi ya wanajeshi wa serikali wanaoshiriki katika operesheni ya kupambana na makundi ya kigaidi wamehusika na mauaji ya kiholela ya makumi ya raia katika eneo la Tillabéri.
Abdullah Sido ameongeza kuwa, habari ya kuuliwa makumi ya raia ambao hawakuwa na silaha ni ya kweli, na kwamba mimaiti za watu wasiopungua 71 waliouawa na askari hao zimepatika katika makaburi sita ya umati.
Amesema kuwa Wanajeshi na Askari Usalama wa Taifa ndio waliohusika na mauaji hayo ya holela.