Serikali mkoani Mbeya imesema kuwa imepata taarifa za badhi ya Vyama vya Siasa kuandaa vijana kati ya 100 na 150 katika kila Kata za Jiji la Mbeya kwa ajili ya kufanya fujo kwenye vituo vya kupigia kura oktoba 28 mwaka huu ili kuharibu mchakato huo.
Hayo yamesemwa na RC Mbeya, Albert Chalamila kwenye kikao na waandishi wa habari ambapo amesema taarifa walizozipata ni kwamba vijana hao watakuwa wanawatisha wapiga kura pamoja na wasimamizi wa uchaguzi pamoja na kufanya maandamano ya kufunga barabara.
Chalamila amesema vyombo vya ulinzi na usalama vipo na vimeandaliwa kwa ajili ya kukabiliana na kundi lolote litakalofanya mambo ya kuhatarisha amani ya mkoa huo vikiwemo vikundi vya vijana hao na kwamba mpaka sasa Mkoa huo uko salama liche ya vitisho vya vikundi hivyo haramu.
Amewataka wananchi wa Mkoa huo kutoogopa wala kutishika na watu hao na badala yake wajitokeze kwenye vituo vyao vya kupigia kura ili watimize haki yao ya kikatiba ya kuwachagua viongozi wanaowataka huku akiwahakikishia kuwa kutakuwa na ulinzi wa kutosha.