Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imetoa muda wa siku tano kuanzia leo Jumatano, Novemba 18, 2020, kwa wanafunzi ambao maombi yao yalikuwa na mapungufu, kurekebisha taarifa zao na kuzituma kwa njia ya mtandao.
Taarifa hiyo imetolewa Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru, wakati akitangaza orodha ya wanafunzi 5,168, wa awamu ya pili wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo.
“Tuna wanafunzi wachache ambao maombi yao yana upungufu ambao kuanzia kesho wataweza kuingia katika akaunti zao za SIPA walizotumia kuomba mkopo na kurekebisha kwa kuweka nyaraka sahihi na tutazifanyia uchambuzi na wenye sifa watapangiwa mikopo mapema iwezekanavyo” Badru
Katika mwaka 2020/2021, Serikali imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 464, kwa ajili ya kugharamia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu 145,000, wakiwemo wanafunzi 54,000 wa mwaka wa kwanza na wanafunzi 91,000 wanaoendelea na masomo.