Mfanyabiashara Ayubu Kiboko na mkewe Pilly Mohammed wamehukumiwa kifungo cha miaka 20 gerezani baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kukutwa na Dawa za Kulevya aina ya Heroin Hydrochloride.
Wawili hao wamehukumiwa leo katika Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu kama Mahakama ya Mafisadi mbele ya Jaji Mfawidhi, Lilian Mashaka.
“Nikizingatia mitigation na sheria za dawa za Kulevya na nikizingatia tangu mlipokamatwa May 23, 2018 na muda wote mlikuwa gerezani na tunafahamu Dawa za Kulevya zina athari, ninawahukumu kutumikia kifungo cha miaka 20 jela na kama hamjaridhika mna haki ya kukata rufaa,” Jaji Mashaka.
Pia Jaji Mashaka ameamuru vielelezo ambavyo ni Dawa za Kulevya viteketezwe, huku vielelezo vingine (Mali- Magari) ya washitakiwa yarudishwe kwa mshitakiwa wa Kwanza na Wapili (Kiboko na Mkewe).
Awali katika hukumu hiyo ikiwa ni kesi ya Uhujumu Uchumi namba 13 ya mwaka 2018 Jaji Mashaka alisema kwamba ushahidi wa upande wa mashitaka umethibitisha kesi kwa mshitakiwa wa kwanza na wapili, hivyo mahakama inawatia hatiani kwa makosa wanayoshitakiwa nayo.
Jaji Mashaka alisema kuwa kwa maoni yake utetezi wa mshitakiwa wa Kiboko na mkewe uliunga mkono ushahidi wa Upande wa Mashitaka kutokana na kujichanganya kwa maelezo yao ya ushahidi.
“Mshitakiwa wa Kwanza na Wapili mlikuwa mnajua kwamba kulikuwa na Dawa za kulevya katika Stand ya Viatu,”
“Mshitakiwa wa Kwanza na Wapili mna makosa kama mlivyoshtakiwa na mna hatia kwa kukutwa na Dawa za Kulevya aina ya Heroin”
Katika kesi ya uhujumu uchumi namba 29/2018, Kiboko na mkewe wanadaiwa, Mei 23, 2018 eneo la Tegeta Nyuki Masaiti wilaya ya Kinondoni, walisafirisha dawa za kuĺevya aina ya heroin zenye uzito wa gramu251.25.