Rais mteule wa Marekani, Joe Biden amesema vitengo muhimu vya usalama vimefanyiwa uharibifu mkubwa chini ya utawala wa Rais Donald Trump.
Biden amesema timu yake haipati habari inazohitaji kutoka kwa idara ya ulinzi wakati ambapo inajiandaa kuchukua mamlaka.
Kiongozi huyo mteule ametoa kauli hiyo wakati akizungumza baada ya kupatiwa habari na Maafisa wa Usalama pamoja na wale wa masuala ya sera za kigeni.
Biden anatarajiwa kuapishwa Januari 20, mwakani kuwa rais, hata hivyo Rais Trump amekataa kukubali kushindwa katika uchaguzi wa mwezi Novemba.
Kwa wiki kadhaa baada ya uchaguzi huo wa Novemba 3, Biden alizuiliwa kupata habari muhimu za kijasusi, ikiwa ni muhimu na utaratibu wa kawaida katika mchakato wa kumkabidhi rais mteule mamalaka.
Kufuatia matamshi ya Biden jana jumatatu , kaimu waziri wa ulinzi, Christopher Miller amesema kwamba maafisa wamekuwa wakifanya kazi kwa utaalamu mkubwa kuunga mkono mpito.