Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul amemtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kuhakikisha kuwa ndani ya siku 7 anamlipa Mkandarasi anayejenga Machinjio ya Vingunguti shilingi Bilioni 5 anazodai ili aweze kukamilisha ujenzi huo.
Gekul ametoa agizo hilo alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa machinjio hayo yaliyopo jijini Dar es Salaam Januari 8, 2021.
Amesema kuwa hali za machinjio nyingi kwa sasa sio nzuri, Wanyama wanachinjwa katika mazingira machafu na sio salama kwa walaji huku akisema machinjio hayo ya Vingunguti yatakuwa mkombozi kwa wananchi wa DSM na Tanzania kwa ujumla.
“Kwa hiyo Mkurugenzi hakikisha ndani ya siku 7 kuanzia leo tarehe 8 unamlipa Mkandarasi ili kazi hii ikamilike kama ambavyo Rais, Dkt. John Magufuli alivyoagiza,” Gekul
Gekul aliendelea kusisitiza kuwa kukamilika kwa ujenzi huo ni lazima uende sambamba na ununuzi wa magari kwa ajili ya kubebea nyama na kuzisambaza katika mabucha yaliyopo jijini Dar es Salaam kwani haitapendeza kuwepo kwa machinjio hayo mazuri halafu nyama ziwe zinabebwa kwenye pikipiki.
Aliongeza kuwa ili kuhakikisha machinjio hayo yanapata Wanyama wazuri na salama kwa ajili ya walaji, wataboresha mnada wa machinjio ya Pugu ili wanyama watakaokuwa wanapelekwa hapo wawe na viwango vya kuchakatwa katika machinjio hayo.
Aidha, aliwapongeza Mkurugenzi na Mkandarasi kwa jitihada kubwa wanazozifanya katika kukamilisha ujenzi huo na kuwataka kuongeza kasi ya ujenzi ili ukamilike kama inavyotarajiwa.
Naye, Msimamizi wa ujenzi huo kutoka Shirika la Nyumba la Taifa, Mhandisi, Efraim Phanuel alisema kuwa endapo watalipwa kiasi hicho cha pesa wanachodai kama alivyoagiza Naibu Waziri watakamilisha ujenzi huo mapema mwezi wa pili mwaka huu.