Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo (Mb) amesema Tanzania itendelea kushirikiana na India katika kuhakikisha mazingira bora ya kibiashara kwa wafanyabiashara pamoja na kuendeleza za uhusiano wa kidplomasia kijamii na kiuchumi katika nchi hizo.
Prof. Mkumbo ameyasema hayo alipokuwa akishiriki katika mkutano kibiashara kwa njia ya mtandao kati ya India na Tanzania Mkutano uliofanyika katika ofisi za Wizara zilizopo Mtumba jijini Dodoma.
Mkutano huo ulilenga kujadiliana kuhusu fursa za biashara zilizopo, kuimarisha ushirikiano wa kibiashara, kubadilishana uzoefu na kuonyesha maeneo muhimu ya biashara kati ya India na Tanzania.
Akiongea katika kikao hicho kilichohudhuriwa na Balozi wa India nchini Tanzania na Balozi wa Tanzania nchini India, pamoja na wenyeviti wa wafanyabiashara katika nchi hizo, Waziri aliwashauri wawekezaji kutoka India kuwa wakiwekeza Tanzania wataweza kuuza bidhaa na huduma zao katika nchi za Afrika Mashariki (EAC) na nchi za Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika(SADC) bila ushuru wa forodha na ukomo wa kiwango cha bidhaa kama ilivyo kwa kwa wafanyabiashara wa Tanzania.
Akiwahimiza wawekezaji kuja kuwekeza Tanzania, Waziri alisema kuwa Tanzania ni mwananchama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yenye ukubwa wa soko lenye idadi ya watu wasiopungua milioni 177. Pia Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya ya Maendelea Kusini mwa Afrika yenye ukubwa wa soko lenye idadi ya watu zaidi milioni 300. Vilevile Tanzania iko katika hatua za mwisho za kukamilisha majadiliano ya uanzishaji wa Eneo huru la Biashara Afrika litakalokuwa na ukubwa wa soko lenye idadi ya watu isiyopungua bilioni 1.5.
“Hivyo, kwa kuzingatia jinsi India ilivyoendelea katika Sekta ya Viwanda na Biashara, nawahimiza wafanyabiashara wa India kuja hususani wenye Viwanda kuwekeza katika maeneo ya fursa zilizopo Tanzania hasa katika uongezaji wa thamani wa mazao ya kilimo, ngozi na madini” Prof. Kitila
Aidha, Prof Mkumbo alizisihi taasisi za Serikali Tanzania na India kufanyia kazi vikwazo vya kibiashara hususan vikwazo visivyo vya kiushuru (non- tariff barriers) ili kurahisisha upatikanaji wa bidhaa na huduma baina ya nchi hizo.