Waziri wa Viwanda na Biashara Profesa Kitila Mkumbo ameielekeza Taasisi ya Wakala wa Usajili wa Bishara na Leseni (Brela) kutokuona sifa kwa watu waofunga biashara.
Prof. Mkumbo ameyasema hayo juzi jijini Dar es Salaam baada ya kutembelea Taasisi hiyo ambapo amesema Brela imepewa jukumu la kuwezesha ufanyaji biashara nchini na sio kudhibiti biashara, hivyo katika utekelezaji wa majukumu amewaelekeza watumishi wa Brela kila wanapopokea taarifa kutoka kwa mfanyabiashara kutaka kufunga biashara au kampuni afuatiliwe kwa ukaribu kujua changamoto iliyopelekea kufikia hatua hiyo.
“Kama taasisi yenye jukumu kubwa tusione sifa kumhudumia mfanyabiashara anayetaka kufunga biashara labda ufungaji huo utokane na migogoro ndani ya kampuni” Prof. Mkumbo
“Unaweza kukuta kwenye kampuni wamegombana kutokana na hisa au mmoja anataka kuzidisha hisa kwenye kampuni kinyemela, hayo yatatuliwe kisheria na kikanuni na sio kutumia busara sana ili kuweza kupunguza migogoro mingi,” Prof . Mkumbo.
Upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa amesema hadi sasa kwa mwaka huu wa fedha kampuni zilizosajiliwa ni 7,148 na malengo ya taasisi ni kufikia usajili wa kampuni 9,528 ambapo hadi sasa usajili umefikia asiliamia 75, ongezeko ambalo limetokana na matokeo ya uboreshaji wa mifumo wa usajili kwa njia ya mtandao.