Mkuu wa wilaya ya kahama mkoani Shinyanga ,Mh.AnamringiMacha amewataka wafanyabishara wa Kahama kuzalisha mchele uliofuata matakwa ya Viwango ili kupata masoko kutoka nje ya nchi.
Kauli hiyo ameitoa leo mjini kahama wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa wasindikaji, wajasiriamali na wadau wa bidhaa ya mchele yaliyoandaliwa na Shirika la viwango Tanzania (TBS) kwa lengo la kuwajengea uwezo wa namna bora ya kuzalisha mchele wenye viwango ili kupata masoko ya ndani na nje ya nchi.
Sambamba na hilo Macha alisema kuwa nia ya serikali ni kuhakikisha wakulima wa kahama wanakuza mitaji yao kwa kuzalisha mchele bora na kuwataka kutochanganya madaraja ya bidhaa hiyo kabla ya kufungasha ili kuleta ushindani katika masoko ya nje.
“Tunatarajia kufungua soko la kimataifa la mchele ambalo litatoa fursa kwenu kuuza mazao yenu kwa urahisi na wafanyabiashara kutoka mataifa ya nje hayataruhusiwa kwenda kununua katika masoko ya ndani ya wilaya na kutoa mwanya kwa wakulima kupata faida kutokana na kilimo hicho,”alisema Macha.
Nae Meneja wa mafunzo na utafiti (TBS) Bw. Hamis Sudi Mwanasala ambaye alikuwa anamwakilisha mkurugenzi mkuu wa (TBS) nchini,amesema kuwa mafunzo hayo yatawawezesha wafanyabiashara na wasindikaji
kuzitambua fursa zilizopo katika soko la kimataifa kwa kuzalisha mchele wenye viwango vinavyotakiwa kitaifa.
“Tumepokea maagizo ya serikali ya wilaya kuhusiana na baadhi ya wazalishaji wa mchele kupaka mafuta mchele kabla ya kuungiza sokoni tunalifanyia kazi kwa kuwaelimisha madhara yake ili kuendelea kulinda viwango vya mchele unaozalishwa nchini,alisema Mwanasala.
Mafunzo hayo yanajumuisha washiriki zaidi ya 100 kutoka wilaya ya kahama na yataendelea katika maeneo ya Bukombe,Geita na Sengerema.