Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo (Mb.) amewahimiza wawekezaji kutoka Sweden kuja kuwekeza Tanzania kwa kuwa ina fursa na rasilimali nyingi, hali ya hewa na mazingira mazuri kwa ajili ya biashara na uwekezaji.
Prof. Mkumbo aliyasema hayo katika Mkutano wa Kibiashara na Uwekezaji kati nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Sweden uliofanyika kwa njia ya mtandao katika ofisi za Wizara zilizopo Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma.
Akiongea katika Mkutano huo, Waziri wa Viwanda na Biashara alieambatana na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe (Mb.), amesema Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Sweden na itaendelea kutekeleza makubaliano mbalimbali ya ushirikiano wa kibiashara kati ya nchi hizo.
Akiwahimiza wawekezaji hao kuja kuwekeza Tanzania, Waziri alisema kuwa Tanzania inafanya jitihada mbalimbali katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ikiwemo sera na sheria kupitia utekelezaji wa “Blueprint”, miundombinu ya usafirishaji nchi kavu,baharini na angani pamoja na kulifanya jiji la Dar es Salaam kuwa jiji kubwa la kibiashara ifikapo mwaka 2025.
“Nawasihi wawekezaji kuja kuwekeza nchini ili kuiwezesha Tanzania kuuza mazao yaliyoongezwa thamani na si malighafi, pamoja na kubadilishana teknolojia ya kisasa kati ya Tanzania na Sweden” Profesa Mkumbo.
Aidha, Profesa Mkumbo aliwahimiza wawekezaji hao kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali Tanzania yenye maliasili nyingi kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira, soko la nchi sita (6) zisizo na bahari zinazohudumiwa na Bandari za Tanzania na upatikanaji wa Ajira kwa urahisi.
Mkutano huo kwa njia ya mtandao, ulihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Biashara na Masuala ya Nchi za Nordic wa Sweden, Waziri wa Wizara ya Ustawi wa Viwanda, Biashara na Ujasiriamali wa Kenya; Waziri wa TEHAMA na Ubunifu wa Rwanda; Waziri wa Biashara, Viwanda na Ushirika wa Uganda; Balozi wa Tanzania nchini Sweden; Balozi wa Rwanda nchini Sweden; na Naibu Amid wa Mabalozi wa Afrika Mashariki nchini Sweden
Wengine waliohudhuria Mkutano huo ni Mwenyekiti wa Kituo cha Biashara cha Sweden Afrika Mashariki (SWEACC), Rais wa Kituo cha Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Katibu Mkuu wa Kituo cha Biashara na Viwanda Uganda; pamoja na Viongozi wengine wanaowakilisha wafanyabiashara na wenye viwanda kutoka Sweden na nchi za Jumuiya Afrika Mashariki.