Sekta ya Nishati na Mawasiliano yaongoza katika Mashauri yanayotolewa na Baraza la Ushindani katika mashauri rufaa 215 kati ya 250 sawa na asilimia 86 yaliyowasilishwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi 2021
Hayo yamesemwa na Mshauri wa Sheria wa Baraza la Ushindani (FCT), Kunda Mkenda, wakati akizungumza na Waandishi wa Habari katika eneo la Baraza la Ushindani lililo ndani ya Banda la Wizara ya Viwanda na Biashara katika Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara (DITF) maarufu Sabasaba yanayoendelea mkoani Dar es Salaam.
Amesema Baraza la Ushindani (FCT) limefanikiwa kutoa uamuzi katika mashauri rufaa 215 kati ya 250 sawa na asilimia 86 yaliyowasilishwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi 2021.
FCT limepata mafanikio hayo, licha ya mlundikano uliokuwapo baada ya muda wa wajumbe ambao ni miaka mitatu kumalizika. Alisemwa
“Kuna kipindi muda wa wajumbe ulikuwa umemalizika, hivyo kukawa na mlundikano wa mashauri, lakini sasa wameteuliwa tayari na wataanza kazi hivi karibuni,” Mkenda
Baraza la Ushindani maarufu, Fair Competition Tribunal (FCT) ambalo Mwenyekiti wake ni Jaji wa Mahakama Kuu anayeteuliwa na Rais, ni taasisi iliyo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara iliyoanzishwa na Serikali ili kupokea, kusikiliza na kuamua kesi za rufaa.
Rufaa hizo ni zile zinazotokana na uamuzi wa Tume ya Ushindani (FCC) na Mamlaka za Udhibiti kama Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Anga (TCAA), Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Huduma za Maji (EWURA), Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (LATRA), Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasilano Tanzania (TCRA) na Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA).
Huku akiwahimiza watu kutembelea banda hilo ili wajue haki zao wanapokuwa wanapata na kutumia huduma mbalimbali zikiwamo za ununuzi na utumiaji wa nishati, mawasiliano na usafiri wa anga na ardhini, Mkenda amesema “Baraza limepewa hadhi ya kimahakama ya utoaji haki katika masuala ya ushindani, udhibiti wa soko na kumlinda mlaji (mtumiaji wa huduma)… uamuzi wa kesi za rufaa na za maombi unaotolewa na Baraza la Ushindani ni wa mwisho.”
Alisema licha ya rufaa za mashauri hayo kutoka katika sekta za nishati, mawasiliano, usafiri wa anga na ardhini sambamba na rufaa zinazotokana na ushindani katika soko, mashauri mengi kati ya hayo yaliyohusu hasa sekta ya nishati kupitia Ewura na sekta ya mawasiliano kupitia TCRA.
“Mashauri mengi yametoka sekta ya nishati kupitia EWURA hususani suala la uchakachuaji wa mafuta ambao uliharibu hata magari na kusababisha kesi nyingi pamoja na hitilafu za umeme zilizosababisha baadhi ya nyumba na vifaa kuungua…” Mkenda.
Mkenda alisema mafanikio hayo yameongeza uwajibikaji katika upangaji bei za nishati ikiwamo ya umeme na usafiri huku kampuni zikiongeza umakini kwa kufuata sheria sambamba na kuongezeka uwazi na ushindani wa bei katika kampuni za simu na uwajibikaji kwenye ushindani katika sekta ya biashara.
“Hii imeongeza ufanisi na uzalishaji; usambazaji wa huduma na bidhaa; imekuza ubunifu na kuwezesha matumizi ya rasilimali yenye ufanisi na yanayomlinda mlaji,” alisema na kuongeza: “Ongezeko hilo limetokana na kuongeza weledi kwa wajumbe na watumishi wa Baraza pamoja kutolewa elimu kwa umma kuhusu shughuli za baraza….”
Akizungumzia malengo ya kimkakati ya FCT kwa mwaka 2021- 2022, Mshauri wa Sheria huyo alisema ni kuanza kutekeleza mpango mkakati mpya wa 2021/2022 hadi 2025/2026 baada ya uliopo kumalizika Juni, 2021.
“Mingine ni kuboresha mazingira na kuongeza kasi ya usikilizaji wa mashauri … FCT limejipanga kuboresha mifumo inayotumika katika usikilizwaji wa mashauri ikiwamo ya kurekodi, kufungua na kusajili mashauri kwa njia ya mtandao.