Polisi nchini Afrika Kusini wamethibitisha kumkamata rais wa zamani wa nchi hiyo, Jacob Zuma baada ya kujisalimisha mwenyewe ikiwa imepita wiki moja tangu alipokutwa na hatia ya kuidharau mahakama kufuatia kesi ya ufisadi iliyokuwa ikimkabili na kuhukumiwa kifungo cha miezi 15 jela.
Usiku wa kuamkia leo Alhamisi Julai 8, 2021, Zuma ameanza kutumikia kifungo chake ambapo baada ya vuta nikuvute alisindikizwa na walinzi wake kwenda gereza lililopo karibu na nyumbani kwake katika jimbo la KwaZulu Natal.
Baadhi ya wafuasi wake waliokuwa wamekusanyika nje ya nyumba yake walielezea kutofurahishwa na kiongozi wao huyo kuhukumiwa kifungo.
Awali polisi walitoa onyo kutaka kumkamata Zuma mwenye umri wa miaka 79 iwapo hatajisalimisha mwenyewe.
Alihukumiwa kifungo hicho baada ya kushindwa kufika mahakamani kusikiliza kesi ya rushwa iliyokuwa ikimkabili.
Hukumu hiyo ambayo ni ya kwanza kwa mtu aliyewahi kuwa rais wa Taifa hilo, ilizua mtafaruku wa kisheria huku muda wa mwisho ukiwekwa wa kujisalimisha kwake baada ya awali kugoma kufanya hivyo.