Kwenye list ya habari kubwa za wiki hii imo hii ya Saif al-Islam Mtoto wa aliyekua Rais wa Libya Muammar Muhammad Abu Minyar al-Gaddafi ambapo baada ya miaka 10 ya ukimya, ameibuka na kusema yupo hai na anataka kurudi kuiongoza Libya na kuliunda upya taifa hilo ambalo sasa limepasuka vipandevipande.
Wiki hii New York Times wamemuhoji Islam mwenye umri wa miaka 49 ambae anasema toka kuuwawa kwa Baba yake October 20 2011 Watu wa Libya wamekua wakiishi kwa kuteseka na hakuna chochote bora walichokipata kutoka kwa Watu wanaoiongoza Libya kwa sasa.
Islam ameahidi kurudi tena kufanya siasa kwenye Taifa lake analolipenda na kuongeza kuwa hakuna tena uhasama kati yake na Watu waliowahi kumfunga jela na kumtesa baada ya Baba yake kuuwawa na sasa Watu hao ni Marafiki zake.
Hata hivyo Saif Al Islam ambae ana PhD aliyoipata London School of Economics amekua akitafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa tuhuma za uhalifu wa kivita akishutumiwa kuchochea mauaji ya Waandamanaji waliokuwa wakipinga utawala wa baba yake.
Muammar Gaddafi aliiongoza Libya kwa karibu miaka 40 na Taifa hilo lilitajwa kuwa na utulivu na Wananchi kuishi maisha bora tofauti na wanayoishi sasa baada ya kuuwawa kwake mwaka 2011 na Waasi kuibuka, Watoto 7 wa Gaddafi waliuwawa kwenye machafuko hayo ya mwaka 2011 lakini Islam alifanikiwa kuepuka kifo.